Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Mhe. William Tate Ole Nasha akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma kuhusu mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU) mwaka 2020 yatakayofanyika kati ya Machi 16 hadi 20 mwaka huu Jijini Dodoma .
Mkurugenzi mkuu wa Idara ya wateja wakubwa Benki ya CRDB Bw. Prosper Nambaya akisisitiza kuhusu Benki hiyo kuendelea kushirikiana na Wizara ya Elimu , Sayansi na Teknolojia katika mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU) mwaka 2020 yatakayofanyika kati ya Machi 16 hadi 20 mwaka huuJijini Dodoma .
(Picha zote na MAELEZO)
…………………………………………………………………………………………….
Na.Alex Sonna,Dodoma
Serikali imesema inatambua umuhimu na mchango wa ubunifu na teknolojia katika kurahisisha na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusu kuanza kwa Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU) 2020, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha amesema mashindano hayo ni moja ya mikakati ya Serikali ya kuibua, kutambua na kuendeleza ubunifu na ugunduzi unaofanywa na watanzania.
“Lengo kubwa la MAKISATU pamoja na kukuza na kusaidia kubiasharisha, yanatoa fursa kwa wabunifu na wagunduzi wa teknolojia mbalimbali kujitangaza na kutangaza kwa wadau ubunifu unaozalishwa,” amesisitiza Ole Nasha.
Ole Nasha amesema MAKISATU inawalenga wabunifu kutoka makundi ya shule za msingi, sekondari, vyuo vya ufundi stadi, vyuo vya kati, vyuo vikuu, Taasisi za utafiti na Mfumo usio rasmi.
Aliongeza kuwa kupitia MAKISATU 2019 Serikali imewaibua na kuwatambua wabunifu wachanga zaidi ya 415 huku wabunifu 60 mahiri wakiendelezwa ili ubunifu wao ufikie hatua ya kubiasharishwa.
Kiongozi huyo ametoa wito kwa watanzania wenye ubunifu mbalimbali kushiriki katika mashindani hayo na amewashukuru Benki ya CRDB kwa kukubali kufadhili mashindano hayo.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Wateja Wakubwa kutoka CRDB, Prosper Nambaya amesema Benki hiyo imeamua kuwa na ushirikiano endelevu na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ili kusaidia kukuza ubunifu unaozalishwa nchini kutokana na kuwepo kwa watu wengi wenye mawazo ya kibunifu yanayopaswa kuendelezwa.