***********************************
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda leo February 05 amethibitisha kupokea kiasi cha Shilingi Milioni 600 zilizotolewa na Rais Dkt. John Magufuli kwaajili ya ujenzi wa Majengo Matano ya Kisasa ya Kituo cha Afya Bunju A kwa lengo la kusogeza huduma karibu na wananchi.
RC Makonda amesema wakazi wa Bunju na maeneo ya jirani waliohitajika kufanyiwa Upasuaji walikuwa wakilazimika kusafiri umbali mrefu hadi Hospital ya Mwananyamala kwaajili ya huduma hiyo na kutokana na umbali mrefu baadhi yao hufariki Dunia wakiwa njiani na wengine kutumia gharama kubwa ya usafiri lakini uwepo wa Kituo hicho sasa wananchi watapata huduma hapo hapo Bunju A.
Aidha RC Makonda amesema ujenzi wa Kituo hicho unatarajiwa kuanza muda wowote kuanzia leo na utachukuwa muda wa miezi mitatu hadi kukamilika ambapo ameielekeza Manispaa ya Kinondoni kuhakikisha inasimamia ipasavyo ujenzi huo.
Pamoja na hayo RC Makonda amesema kukamilika kwa majengo hayo kutafanya Zahanati ya Bunju A kupanda hadhi na kuwa Kituo cha Afya ambapo Serikali imepanga kutoa Madaktari na Wauguzi 58 kwaajili ya kuwahudumia wananchi kituoni hapo.
Hata hivyo RC Makonda amewataka Wananchi wa Kawe kukaa Mkao wa Kula kwakuwa serikali imepanga kujenga Kituo Cha Afya Kata ya Kawe ambapo kukamilika kwa Hospital ya Wilaya ya Mabwepande, Kituo cha Afya Bunju A na Zahanati ya Kawe kutasogeza huduma kwa wananchi.
Kukamilika kwa Kituo hicho kutawezesha Wananchi wa Bunju, Mabwepande, Tegeta, Boko, Mbweni, Kawe, Kunduchi, Madale, Goba na Maeneo ya jirani kuwa na uhakika wa huduma bora za Afya.