*******************************
05 Februari, 2020
Katika kuadhimisha sikukuu ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi Katibu Mkuu wa CCM Dkt. Bashiru Ally amekabidhi mashine ya photokopi yenye thamani ya shilingio milioni moja na nusu kwa mzee Shabani Kanijo (73) ambaye ni mstaafu katika kitengo cha Tehama CCM makao Makuu.
Mzee huyo alikuwa ni mtumishi wa CCM tangu mwaka 1965 na alistaafu mwaka 2004, ambapo baadae alianza kusumbuliwa na maradhi na shughuli zake nyingi za kujipatia kipato zikasismama kwa muda mrefu.
Mapema mwaka huu Mzee Kanijo alifika Ofisi ya Katibu Mkuu kuomba msaada hasa unaohusiana na taaluma yake ili aweze kujimudu na kujiendesha baada ya afya yake kuanza kuimarika, ambapo ombi lake kubwa lilikuwa ni kupata mashine ya kuchapa (Photocopy) kwa ajili ya kufufua steshenari yake iliyokuwa imesimama kwa kipindi chote cha ugonjwa.
Kama ilivyo utaratibu wa Chama Cha Mapinduzi kuwa karibu na makundi mbalimbali ya watu wenye uhitaji hasa wazee, leo tarehe 05 Februari, 2020 Makao Makuu ya CCM, Dkt. Bashiru amemkabidhi vifaa vyote vya steshenari ambapo mzee huyo ameishukuru CCM na kueleza kuwa,
“ninaishukuru sana CCM kwa kuendelea kuwa karibu na sisi wazee, lakini zaidi naipongeza kwa kufanya mambo ambayo wakati wote yalikuwa yakipigiwa kelele na wananchi, sasa hata wapinzania hawana ajenda tena.”
Ameongeza kwa kuuliza kuwa,’’ Hao wapinzania wanataka nini tena? Kama hata wao mambo waliokuwa wanayataka CCM chini ya Rais Magufuli imeyafanya yote.”
Aidha Katibu Mkuu amesisitiza kuwa, ni vema vifaa hivyo ama msaada wowote unaotolewa na Chama utumike kwa malengo yaliotarajiwa na sio vinginevyo ili msaada huo uwe na tija na Chama kiendelee kusaidia wengine zaidi kwa kadri ya uwezo na mahitaji ya wenye uhitaji.
Ikumbukwe kuwa, leo ni siku ya kuzaliwa kwa CCM ambapo Chama hiko kinatimiza miaka 43 tangu kuundwa kwake kutoka vyama vya ukombozi vya TANU na ASP terehe 05 Februari, 1977.