…………………………………………………………………………………….
Na ASP Lucas Mboje, DSM
KAMISHNA Jenerali mpya wa Magereza nchini, Suleiman Mzee(pichani) amewataka Maofisa na askari wote wa Jeshi la Magereza kumpa ushirikiano katika uongozi wake ili aweze kusimamia vyema maelekezo mbalimbali yaliyotolewa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa Jeshi hilo ikiwemo jukukumu la kujitegemea kwa chakula cha wafungwa magerezani.
Akizungumza na Maofisa, askari na watumishi raia wa Jeshi hilo katika Ofisi ndogo za Makao Makuu ya Magereza, jijini Dar es Salaam, Kamishna Jenerali Suleiman Mzee amesema kuwa anayomatarajio makubwa ya kuhakikisha kuwa Jeshi la Magereza linakuwa na miradi mingi ya uzalishaji mali ili kuwezesha kujitegemea badala ya kutegemea bajeti kuu ya Serikali.
“Ni lazima tuzalishe kwa wingi na kila gereza lizalishe kulingana na fursa zilizopo ikiwa tunataka kujiwekea mazingira ya kuaminika. Pia, tuhakikishe kuwa utaalam wetu katika nyanja mbalimbali lazima uwe na manufaa Jeshini”, amesisitiza Jenerali Mzee.
Aidha, Kamishna Jenerali Mzee ameongeza kuwa ni vyema maofisa na askari wa Jeshi hilo wakazingatia utii, uaminifu pamoja na uhodari katika kazi ili kuyafikia matarajio hayo makubwa ndani ya Jeshi.
“Mkizingatia utii, uaminifu pamoja na uhadari katika kazi naamini matokeo chanya yataonekana katika muda mfupi kwani upo uwezekano wa kufanya mambo makubwa ambayo yataliletea heshima na sifa Jeshi letu la Magereza”, amesema Jenerali Mzee.
Kuhusu mafunzo mbalimbali kwa maafisa na askari, amesema kuwa atapitia mitaala ya mafunzo ili kuona kama inaendana na mazingira yaliyopo pamoja na kuifanyia maboresho mbalimbali kwani mafunzo ni nguzo muhimu katika kujenga nidhamu kwa maafisa na askari.
Kwa upande wake aliyekuwa Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike(sasa Balozi Mteule) alimpongeza Jenerali Mzee kwa kuteuliwa na Rais kushika nafasi hiyo na alibainisha baadhi ya changamoto ambazo zinalikabili Jeshi hilo ikiwemo uchakavu wa makazi ya askari.
“Nafurahi kuwa naliacha Jeshi la Magereza likiwa na nidhamu ya hali ya juu pamoja na kuwa na baadhi ya changamoto mbalimbali ikiwemo makazi duni ya askari, naamini changamoto hizo utazifanyia kazi kwani tayari tulikwishaanza kuchukua hatua”, amesema Mhe. Balozi Kasike.
Jeshi la Magereza linamiliki ardhi yenye ukubwa wa ekari 326,205 Tanzania Bara, kati ya hizo ekari 151,350 zinafaa kwa shughuli za kilimo na mifugo. Eneo linalotumika kwa shughuli za kilimo kwa sasa ni ekari 20,580 pekee sawa na asilimia 13.60 ya eneo linalofaa kwa shughuli za kilimo. Jeshi hilo likijipanga kimkakati linaweza kujilisha, kuongeza pato serikalini pamoja na kufanya mapinduzi makubwa ya kilimo hapa nchini.