Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Ofisi ya Hakimu Mkazi Singida, Consolata Singano akihutubia kwenye sherehe za uzinduzi wa maadhimisho ya siku ya sheria mkoani Singida.
Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Mhandisi Jackson Masaka akizungumza kabla ya kufungua rasmi maadhimisho hayo kwa mkoa wa Singida.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida, Yusuph Kasuka akizungumza.
Wadau mbalimbali na Watumishi wa mahakama wakifuatilia matukio mbalimbali wakati wa sherehe za ufunguzi wa wiki ya maadhimisho ya sheria kwa mwaka huu, mkoani Singida.
Wadau mbalimbali na Watumishi wa mahakama wakifuatilia matukio mbalimbali wakati wa sherehe za ufunguzi wa wiki ya maadhimisho ya sheria kwa mwaka huu, mkoani Singida.
Wadau mbalimbali na Watumishi wa mahakama wakifuatilia matukio mbalimbali wakati wa sherehe za ufunguzi wa wiki ya maadhimisho ya sheria kwa mwaka huu, mkoani Singida.
Wadau mbalimbali na Watumishi wa mahakama wakifuatilia matukio mbalimbali.
Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Mhandisi Jackson Masaka, akisisitiza jambo.
Askari wa Usalama Barabarani akizungumza.
Na Mwandishi Wetu, Singida
HAKIMU Mkazi Mfawidhi wa Ofisi ya Hakimu Mkazi Singida, Consolata Singano, amewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kwenye maadhimisho ya wiki ya sheria mkoani hapa, ambapo wadau wote wa mahakama pamoja na watoa huduma wa kisheria watapita maeneo tofauti kuanzia Februari 1 hadi 6 mwaka huu kulingana na utaratibu uliowekwa ili kutoa elimu, sambamba na kusaidia kutatua changamoto mbalimbali za kisheria zinazowakabili
Maeneo yanayotarajiwa kufikiwa ni shule za msingi na sekondari za Pallot Girls, Mughanga, Chief Senge, Nyerere na Ilongero, vyuo, pamoja na stendi kuu ya mabasi, kituo cha afya Sokoine, Gereza la Wilaya, Banda la Mahakama lililopo viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi, radio Standard na eneo la soko kuu
“Nawaomba wakazi wa Singida mjitokeze kwa wingi, ili kupata huduma na taratibu za ufunguaji wa mashauri, Sheria na taratibu zinazotumika katika kuendesha mashauri, Taratibu za mashauri ya mirathi, jinai, mifumo mbalimbali ya TEHAMA-Mahakamani, na mengineyo, hii ni fursa nyingine ya kutatua kero zinazowatatiza kisheria,” alisema Singano na kuongeza:
Mbali na Mahakama, Wadau muhimu wa Mahakama wakiwemo; Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Polisi, Magereza, Uhamiaji na wengine watakuwepo.”
Aidha, Singano alisema maudhui ya Maadhimisho hayo yanaashiria kuanza rasmi kwa mwaka mpya wa shughuli za Mahakama na huwa yanaambatana na kauli mbiu yenye maudhui mahsusi ya kutoa elimu kwa umma juu ya shughuli za utoaji haki. Maudhui ya Mwaka 2020 ni: “Uwekezaji na Biashara: Wajibu wa Mahakama na Wadau kuweka Mazingira wezeshi ya Uwekezaji.’’
Alisema kaulimbiu hiyo inaweka wazi kuwa sheria, utawala wa sheria na mfumo wa utoaji haki kwa wakati ni nyenzo muhimu katika kufanikisha na kurahisisha biashara, uwekezaji, ukuaji wa uchumi na ustawi wa wananchi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Mhandisi Jackson Masaka, ambaye ndiye aliyekuwa mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa wiki ya maadhimisho hayo alisema “Nimejaribu kuhusisha dhima ya mwaka huu na ile kauli ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere inayosema ‘ili uendelee unahitaji watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora’,” alinukuu Masaka
Alisema mahakama nchini ina kazi kubwa sana katika kuhakikisha inatekeleza kauli hiyo kwa kuzingatia kwamba watu bila sheria, watu bila miongozo na watu bila taratibu nchi itageuka kuwa na vurugu, hivyo ni jukumu la mahakama kuwaelimisha watu wajue sheria, na kuwaongoza watu kisheria ili wafanye kazi zao na waheshimu utawala na sheria zilizopo
Aidha, Masaka alieleza sehemu ya kitabu kilichoandikwa na Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamini Mkapa, ‘My Life, My Purpose’ kwamba kulingana na kitabu hicho inaonyesha mara nyingi watu wanapenda kuheshimu mamlaka ya kiutawala kuliko sheria.
Mhandisi Masaka alisema ili watu waendelee ni lazima waongozwe na sheria, huku akisisitiza kuwa ardhi ndio mwanzo wa uwekezaji-huwezi kuwekeza hewani, hivyo katika hilo mahakama inapaswa kusaidia katika kuhakikisha migogoro ya ardhi inamalizika, sambamba na kuwepo na sheria nzuri ambazo hazileti migogoro
“Tusisubiri watu wagombane ili tuonyeshe umahiri wetu katika kusimamia sheria, tuone ni namna gani ya kutoa elimu ili watu wasiwe na migogoro mingi…naomba tutoe sana elimu,” alisema
Akizungumzia suala la siasa safi alisema lazima iendane na sera nzuri, huku eneo la uwekezaji na biashara ni sharti kwanza kuwe na sera nzuri na za kuvutia. Alisema katika hilo serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli imekuwa ikisisitiza juu ya kulegeza masharti mbalimbali, kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji, sambamba na kuwekeza katika biashara, viwanda na miradi mingine ya maendeleo
Alisema kuhusu uongozi bora wadau wa sheria kote nchini wapitie na kuangalia kisheria maeneo yanayowakwaza wawekezaji ili kama itawezekana yaweze kufanyiwa marekebisho
Naye Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida, Yusuph Kasuka, alisema katika maadhimisho hayo kwa mwaka huu wamealika wadau wote muhimu ambao kimsingi ni sehemu ya kutekeleza kauli-mbiu hiyo ya mahakama. Huku akisisitiza kuwa chombo hicho ndio sehemu sahihi ya kutafsiri sheria kwa usahihi na wakati.
“Tukiendelea kuchelewesha haki tunaweza pia kuendelea kuchelewesha uwekezaji…kama tunavyofahamu uwekezaji unahusisha watu, unahusisha ardhi na miundombinu, pia niwasihi watu wasimalize matatizo yao kwa kujichukulia sheria mkononi, wafike mahakamani au kwenye taasisi na mamlaka sahihi zinazoweza kutafsiri sheria,” alisema Kasuka
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini itakayofanyika jijini Dar es Salaam, Februari 06, 2020.