Daktari mbobezi wa moyo na mzibuaji wa mishipa ya damu ya moyo kutoka kampuni ya Medtronic kwa nchi zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara Dkt. Hani Abdel Hadi akiwaelekeza wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) namna ya kuzibua mishipa ya damu ya moyo ambayo imeziba kwa muda mrefu uzibuaji ambao unahitaji utaalamu wa hali ya juu katika kambi maalum ya kufundisha na kufanya matibabu ya siku tatu inayofanyika katika Taasisi hiyo. Jumla ya wagonjwa 12 wanatarajiwa kuzibuliwa mishipa ya damu ya moyo kwa njia ya upasuaji mdogo wa moyo wa bila kufungua kifua kwa kutumia mtambo wa Cathlab (Catheterization Laboratory) ambapo mgonjwa anatobolewa tundu dogo katika mshipa wa damu wa mkono.
Wataalamu wabobezi wa moyo na wazibuaji wa mishipa ya damu ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na mwenzao kutoka kampuni ya Medtronic kwa nchi zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara Dkt. Hani Abdel Hadi wakizibua mishipa ya damu ya moyo ya mgonjwa ambayo imeziba kwa muda mrefu katika kambi maalum ya siku mbili inayofanyika katika Taasisi hiyo. Kampuni ya Medtronic ni watengenezaji na wasambazaji wa vifaa vinavyotumika katika upasuaji na uzibuaji wa mishipa ya moyo wamemtuma mtaalamu huyo katika Taasisi hiyo kwa ajili ya kufundisha na kutoa matibabu yanayohitaji utaalamu wa hali ya juu kwa wagonjwa ambao mishipa yao ya damu ya moyo imeziba.
Picha na JKCI
**********************************
Na Mwandishi Maalum,
Dar es Salaam, 03/02/2020 Jumla ya wagonjwa 12 ambao mishipa yao ya damu ya moyo imeziba kwa muda mrefu (Total Chronic Occlusion – CTO) wanatarajiwa kufanyiwa upasuaji unaohitaji utaalamu wa hali ya juu katika kambi maalum ya matibabu inayofanyika katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Daktari mbobezi wa moyo na mzibuaji wa mishipa ya damu ya moyo wa JKCI Peter Kisenge alisema kambi hiyo ya siku tatu wanaifanya kwa kushirikiana na daktari kutoka nchini Saud Arabia na Shirika la Madaktari Afrika la nchini Marekani.
“Matibabu ya wagonjwa ambao mishipa yao ya damu imeziba na kukaa kwa muda mrefu bila ya kupata matibabu ni magumu na yanahitaji utaalamu wa hali ya juu. Kupitia kambi hii wagonjwa wenye matatizo hayo watapata matibabu”, alisema Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge ambaye pia ni Mkurugenzi wa Tiba ya Moyo alisema aina ya matibabu yanayofanyika ni ya kuzibua mishipa ya damu ya moyo kwa njia ya upasuaji mdogo wa moyo wa bila kufungua kifua kwa kutumia mtambo wa Cathlab (Catheterization Laboratory) ambapo mgonjwa anatobolewa tundu dogo katika mshipa wa damu wa mkono.
“Upasuaji wa aina hii una faida kubwa kwa mgonjwa kwani baada ya matibabu kukamilika anaweza kukaa hospitali kwa muda wa masaa machache na kuruhusiwa kurudi nyumbani bila kulazwa wodini”,.
“Faida nyingine inayopatikana katika kambi hii ni utoaji wa mafunzo ambayo yatawawezesha madaktari kutoka JKCI kuendelea kutoa huduma hizi siku za mbeleni,” alisema Dkt. Kisenge.
Aidha Dkt. Kisenge amewaomba madaktari nchini kutuma wagonjwa waliopo mikoani wenye matatizo ya moyo hasa wenye matatizo ya mishipa ya damu ya moyo iliyoziba ili waweze kupata matibabu sahihi katika Taasisi hiyo.
Kwa upande wake Daktari mbobezi wa moyo na mzibuaji wa mishipa ya damu ya moyo kutoka Shirika la Madaktari Afrika la nchini Marekani Eric Powers alisema madaktari kutoka shirika hilo wamekuwa wakitoa mafunzo ya mara kwa mara kwa wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete na sasa wanatoa mafunzo ya uzibuaji wa mishipa ya damu iliyoziba kwa muda mrefu kupitia mishipa iliyopo kwenye mikono.
“Mabadiliko ni makubwa sana katika utoaji wa huduma za matibabu kwa wagonjwa hapa JKCI, mafunzo ya mara kwa mara yameboresha huduma za matibabu na kuwafanya wataalamu wa Taasisi hii kuweza kumudu kufanya upasuaji wa aina mbalimbali wa magonjwa ya moyo hapa nchini”, alisema Dkt. Powers.
Kambi hiyo inayoenda sambamba na utoaji wa mafunzo kwa wataalamu wa Taasisi hiyo imedhaminiwa na Kampuni ya Medtronic kwa nchi zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara ambao ni watengenezaji na wasambazaji wa vifaa vinavyotumika katika upasuaji na uzibuaji wa mishipa damu ya moyo.