Katibu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Raya Issa Msellem akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu kuanza kwa Mkutano cha 17 wa Baraza la Wawakilishi ,huko katika ukumbi wa Baraza la wawakilishi ,Chukwani Zanzibar .
Baadhi ya Waandishi wa Habari wakimsikiliza Katibu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Raya Issa Msellem (hayupo pichani) kuhusu kuanza kwa Mkutano cha 17 wa Baraza la Wawakilishi, huko katika ukumbi wa Baraza la wawakilishi ,Chukwani Zanzibar .
………………………………………………………………………………………………………
Na Kijakazi Abdalla,Maelezo
Mkutano wa kumi na saba wa Baraza la Tisa la Wawakilishi Zanzibar unatarajiwa kuanza siku ya Jumatano tarehe 5/02/2020 huko Chukwani nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Hayo ameyasema Katibu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Raya Issa Msellem huko katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu kuanza kwa Mkutano huo .
Amesema katika Mkutano huo jumla ya Maswali 112 yameratibiwa kwa ajili ya kujibiwa kwenye mkutano huo.
Aidha amesema miswada ya Sheria iliyowasilishwa na kusomwa mara ya kwanza katika mkutano wa Disemba ,2019 itasomwa kwa mara ya pili na kujadiliwa katika Mkutano wa kumi na saba.
Katibu huyo wa Baraza amesema Miswada hiyo ni Mswada wa Sheria ya kufuta Sheria ya Mawakili, sura ya 28 na Sheria ya Wakuu wa Viapo sura ya 29 pamoja na kutunga sheria ya Mawakili na mambo mengine yanayohusiana na hayo.
Pia amesema kutasomwa Mswada wa Sheria ya kuweka masharti yanayohusiana na Haki na Huduma za Ustawi kwa Wazee,na kuanzisha Mpango wa Pensheni Jamii,Usimamizi wake na mambo mengine yanayohusiana na hayo.
Vilevile amesema Uwasilishwaji wa Ripoti za Kamati za Kudumu za Baraza la Wawakilishi kwa Mwaka 2019/2020 ,Mwelekeo wa Mpango wa Taifa na pia kutawasilishwa taarifa za Dawa za Kulevya kwa mwaka 2018.