Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akisema jambo kwa wadau wa Sekta ya Afya (hawapo pichani) katika siku ya Saratani Duniani iliyofanyika katiaka Taasisi ya Saratani ya Ocean Road.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (wa pili kutoka kushoto) akionyesha mwongozo wa matibabu ya saratani nchini Tanzania mara baada ya kuuzindua katika siku ya Saratani Duniani iliyofanyika katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akizindua mwongozo wa matibabu ya saratani, upande wa kulia ni Mkurugenzi wa Huduma za Tiba kutoka Wizara ya Afya Dkt. Grace Maghembe, aliye kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji Taasisi ya Saratani ya Ocean Road Dkt. Julius Mwaiselage
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akikabidhi mwongozo wa matibabu ya saratani kwa Mkurugenzi Mkuu Taasisi ya Mifupa MOI Dkt. Respicious Boniface.
******************************
Na Mwandishi Wetu – Dar Es Salaam
Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imezindua mwongozo wa kitaifa wa tiba ya magonjwa ya saratani utakaoziwezesha hospitali za serikali na binafsi katika kutoa matibabu kwa usawa na kurahisisha mawasiliano kati ya madaktari bingwa na wataalamu wengine.
Kuzinduliwa kwa mwongozo huo kumefuatia baada ya hospitali za kanda kuanza kutoa tiba za saratani, kuongezeka kwa hospitali binafsi na za umma zinazotibu ugonjwa huo kwa sasa nchini, huku kwa kipindi kirefu hospitali nyingi zikitumia miongozo tofauti na ile ya nje ya nchi.
Akizindua mwongozo huo, Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema huduma za saratani zinasambaa katika hospitali mbalimbali nchini kwa sasa hivyo utoaji wa huduma lazima uangaliwe ili zitoke kwa kiwango kinachopaswa.
Amesema kuwepo kwa miongozo tofauti ilisababisha kutokuwepo kwa usawa katika tiba za wagonjwa lakini pia kulikuwa na changamoto ya mgonjwa kuendelea na tiba sahihi pindi akipewa rufaa kwenda hospitali nyingine.
“Kuwepo kwa mwongozo huu kutawezesha kurahisisha mawasiliano kati ya madaktari bingwa na wataalamu wengine wa matibabu ya saratani kote nchini,
“Kurahisisha uandaaji wa maoteo na ununuzi wa dawa na vitendanishi vinavyotumika katika matibabu ya saratani, mwongozo huu pia umetoa orodha ya dawa na vifaa tiba kwa ajili ya matibabu ya saratani ambayo itatumika kama mwongozo kwa ajili ya manunuzi na matumizi nchini,” amesema Ummy Mwalimu.
Amesema mwongozo huo pia itawezesha wananchi kupata huduma bora na za viwango vya juu katika vituo vyote vya matibabu kwa kuwa tiba zote zitapangwa kwa kufuata mwongozo huo.
Waziri Ummy amesema pia utawezesha kutoa mwongozo kwa mfuko wa taifa wa bima ya afya NHIF kuhusu dawa na vipimo mbalimbali stahiki kwa wagonjwa wa saratani.
“Mfuko wa Taifa NHIF uhakikishe unatumia mwongozo huu katika kuweka vitita vya huduma za saratani hapa nchini kwani katika ile standard treatment guideline kuna baadhi ya dawa za kutibu saratani hazikuorodheshwa, na niwaambie mmeweka masharti magumu sana katika vipimo hivi CT Scan na MRI nani anapima mara kwa mara tuondoe baadhi ya vikwazo na hili NHIF mkalitekeleze,” ameagiza.
Ameagiza mwongozo huo utumike na vituo vyote vinavyotoa tiba za saratani nchini;
“Ninafahamu hospitali zote zilishiriki kuuandaa hivyo sitegemei kusikia kuna hospitali inafanya tiba nje ya mwongozo huu, ninaagiza pia wizara kufanya mapitio ili kuhakikisha dawa zote zinazotibu saratani zinakumuishwa katika mwongozo huu.”
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) Dk Julius Mwaiselage amesema, “Matumizi ya mwongozo huu yamefanyiwa majaribio kwa kipindi cha miezi sita katika taasisi hii kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha St Francisco.”