Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) akijibu swali bungeni Jijini Dodoma leo tarehe 3 Februari 2020 wakati wa mkutano wa kumi na nane.
……………………………………………………………………………………….
Na Mathias Canal, Wizara ya kilimo-Dodoma
Kutokana na kuwepo kwa upungufu wa pembejeo nchini, Serikali imechukua hatua mbalimbali za kuhakikisha pembejeo zinapatikana kwa wingi ili kutosheleza mahitaji ya ndani ya nchi.
Hatua hizo ni pamoja na; kutoa vibali kwa wasambazaji wakubwa wa mbolea kuagiza nje ya mfumo wa BPS kutokana na mahitaji ya wakulima na soko ambapo tani 200,000 zimeagizwa na hadi kufikia tarehe 30 Januari, 2020; Kutoa kibali cha kuagiza tani 45,000 kwa Umoja wa wasambazaji na wauzaji wa pembejeo za kilimo; na kuagiza mbolea tani 43,000 kwa kutumia mfumo wa BPS ambapo mbolea hiyo imeanza kusambaza nchini tangu tarehe 28 Januari, 2020.
Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) ameyasema hayo tarehe 3 Januari 2020 bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Kavuu Mhe Dkt. Pudeciana Wilfred Kikwembe aliyetaka kufahamu serikali ina mpango gani juu ya ucheleweshwaji wa pembejeo za kilimo hasa mbegu na mbolea ambazo huwasababishia wakulima hasara.
Mhe Mgumba amesema kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau inaendelea kuboresha mifumo ya uzalishaji, udhibiti na usambazaji wa pembejeo nchini ambapo sekta ya Umma na binafsi zitashirikishwa na kuhamasishwa kuzalisha pembejeo nchini ili kukidhi mahitaji.
Kuhusu upungufu wa mbolea nchini Mhe Mgumba amesema kuwa umechangiwa na sababu mbalimbali ikiwemo kuchelewa kupatikana kwa mahitaji kutoka kwa Makampuni ya mbolea hapa nchini, kuongezeka kwa matumizi ya mbolea kutokana na bei nzuri ya mazao kwa msimu wa 2018/2019; kuongezeka kwa kilimo cha kibiashara baada ya Serikali kuwahakikishia wakulima kuwa haitafunga mipaka na kuingilia upangaji wa bei za mazao ya kilimo na kuwepo kwa mvua nyingi ambazo zimesababisha kuongezeka kwa viwango vya matumizi ya mbolea kwa wakulima.
Katika msimu wa 2019/2020 upatikanaji wa pembejeo zikiwemo mbegu bora hadi kufikia Desemba, 2019 ni tani 71,155.13. Kati ya hizo, tani 58,509.9 zimezalishwa nchini, tani 5,175.79 zimeingizwa kutoka nje ya nchi na tani 7,469.44 ni bakaa ya msimu 2018/2019.
Aidha, upatikanaji wa mbolea hadi kufikia tarehe 30 Januari, 2020 ni tani 410,499 zikijumuisha tani 92,328 za UREA na tani 84,311 za DAP. Kati ya hizo tani 225,417 zimeingizwa kutoka nje ya nchi, tani 16,685 zimezalishwa ndani ya nchi na tani 168,397 ni bakaa ya msimu wa 2018/2019.