********************************
Na Mwandishi Wetu, Mara
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara, Samuel Kiboye (Namba Tatu) amemtaka Mbunge wa Kigoma Mjini na Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe kuacha chuki binafsi dhidi ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt.John Magufuli.
Amesema barua Zitto aliyoiandikia bodi ya wakurugenzi wa Benki ya Dunia hivi karibuni kwa ajili ya kuicheleweshea Serikali mkopo wa zaidi ya shilingi trilioni moja kwa ajili ya kuboresha elimu, ni jambo mbalo linaonyesha chuki binafsi kwa Serikali.
“Sikufikiria kama ndugu Zitto ambaye ni msomi mwenye uelewa mpana wa mambo angeandika barua ile, ndiyo maana ni vema kabla ya kufanya uamuzi wa namna yoyote lazima ujipe tafakari ya kutosha kwanza.
“Hatua ile inanyesha ni kwa namna gani ndugu Zitto anataka sifa za bure kwa nchi za Ulaya, ila atambue kuwa hakuna Mzungu ambaye ana urafiki wa kudumu na mtu, wao uyapa kipaumbele maslahi yao kwanza, hivyo hali ile ilidhirisha ni kwa namna gani ana chuki binafsi dhidi ya Serikali ya Awamu Tano, lakini atambue kuwa hakuna wa kuikwamisha Serikali yetu, sisi wananchi tumeamua iwe jua au mvua kushirikiana nayo ili kuharakisha maendeleo,”alifafanua Kiboye.
Pia aliainisha kuwa, kuna makundi mengi ya Watanzania ndani na nje ya nchi ambao wanadhamira mbaya kwa juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Magufuli, lakini yatambue kuwa kwa maombi ya Watanzania na kufanya kazi kwa bidii njama zao hazitafanikia.
“Kila jambo analotekeleza Mheshimiwa Rais Magufuli wao wanaona halina faida, walianza na ndege, baada ya kuona zinakuja kwa kasi na matengenezo makubwa ya viwanja vya ndege,wakahamishia lawama miradi ya reli na Mradi wa Ufuaji Umeme katika bwawa la Julius Nyerere, ambayo unatekelezwa kwa fedha za ndani,wao kazi kushinda mitandaoni muda wote kuilamu Serikali, niwaambie huo ni utoto, kila mmoja aonyeshe uzalendo na kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali yetu ili kutuletea maendeleo. Na watabakia kushangaa sana maana kila mradi utafanikiwa licha ya mapingamizi yao,” alifafanua Kiboye.
Wakati huo huo, Kiboye alimpongeza Rais Dkt.Magufuli kwa kuendelea kuwa na moyo wa ujasiri katika kuwatumikia Watanzania, licha ya vikwazo vingi anavyotengenezewa na wenye chuki binafsi.