Home Mchanganyiko KLABU YA KUSOMEA VITABU YAZINDULIWA ZANZIBAR

KLABU YA KUSOMEA VITABU YAZINDULIWA ZANZIBAR

0

Mkurugenzi wa Maktaba kuu Sichana Haji Foum akitoa hotuba ya makaribisho katika hafla ya Uzinduzi wa Klabu ya kusoma Vitabu katika Ukumbi wa Maktaba kuu Mpirani Akrotanal mjini Zanzibar.

Mwenyekiti wa Bakiza Dk Mohamed Seif Khatib akizungumza machache katika hafla ya Uzinduzi wa Klabu ya kusoma Vitabu katika Ukumbi wa Maktaba kuu Mpirani Akrotanal mjini Zanzibar.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Riziki Pembe Juma akitoa hotuba ya uzinduzi wa Klabu ya kusoma Vitabu  iliofanyika  katika Ukumbi wa Maktaba kuu Mpirani Akrotanal mjini Zanzibar.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Riziki Pembe Juma akisisitiza jambo wakati akitoa hotuba ya uzinduzi wa Klabu ya kusoma Vitabu  iliofanyika  katika Ukumbi wa Maktaba kuu Mpirani Akrotanal mjini Zanzibar. 

Mwenyekiti wa Klabu ya kusoma Vitabu Bimaryam Hamdani akitoa hotuba na kumkaribisha mgeni Rasmi  katika hafla ya Uzinduzi wa Klabu ya kusoma Vitabu katika Ukumbi wa Maktaba kuu Mpirani Akrotanal mjini Zanzibar.

PICHA NA YUSSUF SIMAI/MAELEZO ZANZIBAR.
**************************

Na Khadija Khamis –Maelezo- Zanzibar  01/02/2020.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Riziki Pembe Juma amewataka wanafunzi wa skuli mbali mbali za Zanzibar pamoja na jamii kiujumla kuitumia Maktaba Kuu ya Zanzibar kwa lengo la  kujiongezea uwelewa pamoja  na ufahamu wa mambo mbali mbali ikiwemo  historia ya nchi .

Hayo aliyasema huko katika Ukumbi wa Maktaba kuu Maisara wakati wa Uzinduzi wa Klabu ya kusomea vitabu yenye lengo la kuihamasisha jamii kupendelea kusoma vitabu.

Amesema kufanya hivyo kutasaidia kujiongezea taaluma na kuirejesha hadhi  ya  awali iliyopotea  ya utamaduni wa kusoma vitabu kwa kuimarisha lugha ya Kiswahili na nyenginezo za kigeni .

Aliwataka wananchi kujiunga na Klabu hiyo ili kuongeza uwelewa wa mambo tofauti ikiwemo mambo ya kihistoria, utamaduni,kisiasa,kiuchumi, kiufundi,  kilimo na mengine mengi .

“Waliyafanya waliyaandika tunayasoma  na kuyajuwa na kuridhisha vizazi vijavyo kama vile Mapinduzi ya Zanzibar wengi tulikuwa hatujazaliwa lakini tumesoma vitabu tumejuwa hii ndio hazina moja kubwa sana “, alisema Waziri wa Elimu

Aidha alisema ushajihishaji wa kujisomea vitabu kwa wanafunzi kutawasaidia katika mitihani yao na wataachana na simu ambazo hawazitumii ipasavyo jambo ambalo linazorotesha  maendeleo yao ya kielimu .

Alifahamisha kuwa kuna vitabu vingi  vizuri vya zamani ambavyo wanafunzi hawavijui kama vile Alfu ulela ulela,Mzimu wa watu wa kale na vyengine vingi iko haja kuvisoma na kuvielewa dhamira ya mtunzi aliyoikusudia ambayo ina ujumbe kwa jamii na vizazi vijavyo kupitia tahakiki mbali mbali zinazofanywa na wataalamu wa klabu hiyo .

Hata hivyo Waziri huyo alitoa rai kwa jamii kutumia wigo za tamaduni za kigeni za kubeba vitabu na kuvisoma katika safari zao kama vile katika ndege na safari za masafa marefu .

.

Nae Mwenyekiti wa Bakiza Dkt. Mohamed Seif Khatib alisema zamani maktaba iliitwa jengo la wajinga kwa maana ya kwamba ukitaka upunguze  ujinga ufike kujisomea vitabu mbali mbali uweze kupata uwelewa mpana wa mambo  .

Alisema elimu nzuri ya kujiimarisha ni kununua vitabu mbali mbali kwa kuweka maktaba majumbani kufanya hivyo kutasaidia wanafunzi   kujisomea vitabu hivyo .   

Aliwafahamisha wanafunzi kuwa na muamko wa kusoma vitabu na kuvielewa sio kuhifadhi uhakiki  jambo ambalo linasababisha kushindwa  kuingiza mawazo yao katika kujibu mitihani.

 “wanafunzi wanakunywa uhakiki mwanzo mwisho wakati wa mitihani wanacheuka vile vile hii haipendezi kwasababu wanatakiwa waingize mawazo yao kwa  mujibu walivyokisoma kitabu hicho”, alisema Dkt Mohamed.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Klabu hiyo Bi Mariamu Hamdani alisema kuwa  tabia ya kusoma vitabu inaadhiri kutoweza kuiacha pindipo ukiizowea na hukufanya uwe na uwelewa mpana wa kujuwa mambo mengi kupitia usomaji wako wa vitabu mbalimbali .

Alifahamisha Clabu hii itafanya uhakiki wa vitabu  mbali mbali kwa kuanzia na kitabu cha Bwana Msa, “Mzimu wa watu wa kale”  lengo ni kuihamasisha jamii kutaka kuufahamu  mzimu huu umefanya nini kupitia maktaba za vitabu hivyo

Alifahamisha wataendelea kuhakiki vitabu kupitia klabu hiyo ili kuwawezesha wanafunzi na jamii kuvifahamu vitabu hivyo kwa ufasaha na  kujuwa dhamara ya Mtunzi kwa jamii katika harakati ya kutoa elimu kupitia fasihi andishi .

Klabu ya kusoma vitabu imeanzishwa Oktoba mwaka jana ikiongozwa na Mwenyekiti wa Klabu hiyo Bi Mariam Hamdan na Katibu Dkt Mwanahija Ali Juma .