***********************************
Happy Lazaro,Arusha.
Kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika mikoa mbalimbali nchini zimeendelea kuleta madhara ikiwemo ya kambi za watalii wanaolala katika eneo la Mto wa mbu wilayani Monduli kutokana na eneo hilo kufurika maji na hivyo kuleta hofu kubwa miongoni mwa wananchi hao.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti Wakazi wa mji Mdogo wa Mto wa Mbu wilayani Monduli mkoani Arusha eneo la Migungani A wameiomba serikali kunusuru maisha yao na hatari ya kusombwa na mafuriko kutokana na kukosekana miundombinu imara inayoruhusu maji ya mvua kutiririka ambayo yamekuwa yakikosa muelekeo hivyo kutuama katika makazi,shule na kusababisha hofu kubwa kwa maisha yao na hata kambi za watalii wanaolala eneo hilo kufurika maji.
Tangu mvua zimeanza kunyesha katika msimu huu wakazi hao wamekuwa wakikumbana na adha kubwa ya maji kujaa katika nyumba zao,mashamba,shule ambapo hali imezidi kuwa mbaya zaidi pale baadhi ya kambi za watalii nazo kuonekana kujaa maji ,hivyo kusababisha wageni kushindwa kulala katika eneo hilo.
Mmoja wa wakazi hao ,Catherine Kubena, Dotto Mahimbo na mhandisi Kubene Joseph walisema hali imeendelea kuwa mbaya kila kukicha huku wakihofia mvua zinazoendelea kunyesha huenda zikaleta madhara Zaidi.
“Yaani sasa hivi mvua ikinyesha watu hatuelewi tutoke nje au tubaki ndani maana maji yanajaa vitu vinaharibika hata hatulali usingizi kweli maisha yetu yapo hatarini tunaomba serikali iingilie kati suala hili kwa kutuongezea makalavati ili tuweze kuishi kwa Amani”wananchi.
Aidha wananchi hao,walisema kuwa kukosekana kwa makalavati ya kutosha na mifereji ambayo inaonekana myembamba ikishindwa kuhimili kiwango cha maji yanayotiririka lakini pia baadhi ikiwa imeziba ndio haswa chanzo cha tatizo lote hili,ambapo wananchi hawa wanaamua kupaza sauti zao baada ya hali kuendelea kuwa mbaya.
Hata hivyo ,Sekta ya utalii nayo imeonekana kuathirika Zaidi ambapo Baadhi ya maeneo yaliyoathirika Zaidi ni kambi ya kulala wageni ambazo zimejaa maji hivyo kusababisha wageni kushindwa kulala katika kambi hizo.
“mifereji imeziba,mingine haina uwezo wa kupitisha maji hivi unavyoona hali ni mbaya sana harufu ya maji yamejaa kila mahali na tunahofia afya zetu huenda wakati wowote pakatokea mlipuko wa magonjwa ya tumbo maana mashimo ya vyoo yanazibuliwa kipindi hiki cha mvua.”alisema Janeth
Hata hivyo wakati wakisubiri msaada wa serikali wananchi hao wameamua kujiongeza kwa kujitolea kwa nguvu zao kuanza kuzibua mitaro ya maji lakini bado wanakabiliwa na changamoto ya vitendea kazi duni.