******************************
Waziri wa ulinzi na jeshi la kujenga taifa Dkt. Hussein mwinyi amesema Tanzania itaendelea kuwa mstari wa mbele katika kulinda amani kwenye mataifa yenye machafuko kwa kupeleka vikosi vyenye uwezo wa hali ya juu ili kuhakikisha amani inatawala duniani.
Ameyasema hayo leo jijini Dar es salaam katika hafla ya upokezi wa vifaa vya kijeshi vinavyotumika katika mchakato wa kulinda amani vilivyotolewa na Serikali ya Marekani.
Akizungumza katika hafla hiyo Dkt.Mwinyi amesema kuwa nchi ya Tanzania na Marekani zimekuwa na ushirikiano wa karibu kupitia majeshi pamoja sekta mbalimbali ikiwemo maswala ya kijamii,uchumi na elimu.
“Msaada huo utasaidia kuongeza uwezo wa vikosi maalumu vya kulinda amani katika kukabiliana na changamoto za kulinda amani duniani ikiwa ni pamoja na kuwa na uwezo wa kukabiliana na majanga ya dharula yanayotekea hapa nchini na kuongeza thamani ya jeshi”.Amesema Dkt.Mwinyi.
Kwa upande wake Kaimu Balozi wa Marekani hapa nchini Bw. Inm Patterson amesema kwa takribani mwaka mmoja vikosi vya Tanzania vimeweza kupatiwa mafunzo ya kuviendesha na kuvitumia vifaa hivyo, hivyo ni jukumu lao jeshi kuvitunza na kuweza kusaidia wananchi katika majanga mbalimbali na kuendelea kurfanya mazoezi ili kuweza kukabiliana na jambo lolote linaloweza kujitokeza.
Pamoja na hayo Mkuu wa majeshi ya ulinzi nchini Jenerali Venance Mabeyo amesema kuwa vifaa hivyo walivyokabidhiwa na Marekani ni kuunga mkono jitahada za jeshi la Tanzania katika kulinda amani na vitasaidia vikundi vya jeshi kutoa msaada wa haraka kwa wenye uhitaji.
Aidha vifaa vilivyokabidhiwa leo katika hafla hiyo ni pamoja na magari,jenereta,jiko maalumu,mashine ya kusafishia maji vyenye jumla ya thamani ya dollar millioni 18.