Mkuu wa Wilaya ya Kinondo ,Mhe. Daniel Chongolo akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kuanza kwa zoezi la ulipaji kodi za majengo, kulia ni Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Ndugu. Aron Kagurumjuli na kushoto ni Meneja wa TRA Mkoa wa Kinondoni Bwana Masawe Masaka.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Ndugu. Aron Kagurumjuli akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kuanza kwa zoezi la ulipaji wa kodi za majengo, katikati mwenyesuti nyeusi ni Mkuu wa Wilaya ya Kinondo ,Mhe. Daniel Chongolo.
********************************
Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni leo imezindua zoezi la uhamasishaji wananchi kulipa kodi ya majengo kwa kipindi cha mwaka 2019 / 2020 kitakacho malizika Juni 30 mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Daniel Chongolo amesema kuwa kwa kipindi cha mwaka huu wa fedha wananchi wengi bado hawaja hamasika vya kutosha kwenda kulipa kodi hiyo na kwamba iwapo watachelewa watalazimika kulipa na riba.
Mhe. Chongolo amesema kuwa Rais Dk. John Pombe Magufuli alipokutana na viongozi wa juu kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA mwakajana alitoa maelekezo na hivyo kushusha kiwango cha tozo hiyo ambapo mwananchi mwenyenyumba ya kawaida atalipa kiasi cha shilingi 10,000 huku mwenyenyumba ya Ghorofa kiasi cha shingili 50,000.
Mhe. Chongolo amefafanua kuwa “ kwa wale wenye nyumba za Ghorofa wanalipa kiasi cha shilingi 50,000 kwa floo, kama zipo floo 10 maana yake analipa shilingi 500,000, kama zipo 20 inamana atalipa shilingi 1,000,000, kwa hiyo unaweza kuona“ kodi hii imeshuka kwa kiwango ambacho hakuna mwanachi ambaye hataweza kuilipia” amefafanua.
Aidha Mhe. Chongolo ameeleza kuwa Wilaya ya Kinondoni inajumla ya kaya zaidi ya 340,000 na kwamba iwapo kila kaya italipa kodi hiyo itakuwa imekusanya kiasi cha zaidi ya shilingi Bilioni 3.5 pesa ambazo zinaweza kutumika kwa ajili ya kupeleka huduma kwa wananchi ikiwemo barabara, miundombinu ya maji pamoja na huduma nyingine za msingi.
Hata hivyo Mhe. Chongolo amesisitiza kuwa hadi kufikia Juni 30 mwaka huu asilimia 100 ya wakazi wa Kinondoni wawe wameshalipa kodi hiyo na kwamba taarifa hiyo itapelekwa kila Kata kwa ajili ya kuhamasisha wananchi wengi huku wakifuatilia wale waliokuwa na malimbikizo ya madeni ya nyuma.
“ Niwasisitize wananchi wa Kinondoni, wakati ni sasa na kwamba kama utakiuka sheria hii kuna hatari ya kupoteza jengo lako, tuache tabia ya kusubiria tarahe za mwisho kama ambavyo watu walifanya kwenye usajili wa laini za simu kwa kutumia alama za vidole, niwasihi anzeni kulipa sasa” amesisitiza.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Ndugu. Aron Kagurumjuli amesema kuwa lengo la Serikali ni kukusanya mapato ya kutosha ili iwe na uwezo mkubwa wa kuwahudumia wananchi na hivyo kuwasisitiza wakazi hao kujitokeza kulipa bila kusubiri tarehe za mwisho.
Amefafanua kuwa “awali Halmashauri ilikuwa ikikusanya kodi ya majengo kabla ya kuhamishiwa TRA, ila bado lengo la Serikali ni lile lile la kukusanya mapato na ndio mana na mimi niko hapa, kwa sababu Halmashauri na TRA hakuna tofauti bado ni Serikali ile ile yenye lengo moja la kuwahudumia na kuboresha huduma za wananchi.
Naye Meneja wa TRA Mkoa wa Kinondoni Masawe Masaka amewataka wananchi kuchangamkia fursa iliyotolewa na Rais Dk. Magufuli yakulipa kodi hiyo na kwamba wasisubiri kulipishwa faini pindi watakapo shindwa kulipa kwa wakati.