*****************************
NA EMMANUEL MBATILO
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe.Daniel Chongolo amefurahishwa na kasi ya mradi wa ujenzi wa nyumba za Magomeni Kota hivyo amewataka Wakala wa Majengo TBA kuendelea na kasi hiyo ili waweze kumaliza ujenzi huo mapema.
Akizungumza na wanahabari baada ya kutembelea mradi huo DC.Chongolo amesema kuwa ameridhishwa na kasi ambayo wanaenda nayo TBA katika ujenzi huo, kwani kuna utofauti mkubwa toka alivyofika kwa mara ya mwisho.
“Kuna mabadiliko makubwa toka nilivyokuja mwaka jana mwezi wa kumi mwishoni na sasa, tumeona wameshaanza kuweka na aluminium kwenye baadhi ya majengo pamoja na upakaji wa rangi” Amesema DC.Chongolo.
Aidha DC.Chongolo amewasisistizia TBA waendelee na kasi kwenye ujenzi huo ili angalau mapema ikiwezekana wawe wamemaliza ujenzi huo maana nyumba hizo zinahitajika kwa haraka.
Nae Meneja Mradi wa ujenzi huo Bw. Benard Mayemba amesema kuwa wananednelea na ujenzi kwa kasi kwani wanafanyakazi usiku na mchana ili kufikia mwezi Aprili mwaka huu wawe wameshamaliza ujenzi huo.
“Ni gharama kufanikisha ujenzi huu lakini wakala wa majengo ukishirikiana na serikali tumekuwa tukizalisha vitu mbalimbali ambavyo vitapunguza gharama za ujenzi moja wapo ni kuanzisha kiwanda cha kuchakata zege pamoja na kufyatua matofali hivyo na kuongeza nafasi za ajira kwa wakazi waliopo karibu na ujenzi huo”. Amesema Bw.Mayemba.
Ujenzi huo mpaka sasa upo kwenye asilimia 69 kutekeleza mradi huo ambapo inategewa kumalizika mwezi Aprili mwaka huu kwa mujibu wa wakala wa majengo TBA.