Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila, Dkt. Julieth Magandi akizungumza na Mzee Lucian Komba (kushoto) pamoja na mwanae Adrian Komba (kulia) waliofika hospitalini hapa kushukuru kwa matibabu waliyopata.
Adrian Komba (kushoto) na baba yake mzee Lucian Komba wakieleza jinsi walivyopatiwa matibabu hospitalini hapa.
Dkt. Magandi pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi MNH-Mloganzila, Sr. Redemptha Matindi wakipokea shukrani hizo.
Dkt. Magandi akiagana na Mzee Lucian Komba aliyepatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila na kupona kabisa.
………………………………………………………………………………………………………
Adrian Lucian Komba ameishukuru Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila kwa kumpatia matibabu baba yake Mzee Lucian Anthony Komba na kupona kabisa.
Mzee Lucian Anthony Komba alipokelewa MNH-Mloganzila tarehe 14 Januari, 2020 kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro baada ya kuanguka na kupata jeraha sehemu ya kichwa lililopelekea hali yake kuwa mbaya.
Baada ya kupokelewa hospitalini hapa alipatiwa matibabu na wataalam wa upasuaji wa mishipa ya fahamu na kukaa hospitalini kwa muda wa wiki tatu na kuruhusiwa kurudi nyumbani akiwa amepona kabisa.
Akizungumza wakati wa kushukuru Adrian Anthony Komba alisema baba yake amepona kabisa jambo ambalo limewashangaza hata watu waliomuona baba yake wakati wa ugonjwa.
“Naishukuru Hospitali ya Mloganzila na watoa huduma kwa matibabu haya kwa sababu nilimleta baba kwa rufaa akiwa hajitambui leo namuona anaongea ni jambo la kufurahisha, hata watu waliomfahamu wakati wa ugonjwa tuliporudi anaongea walimshangaa” amesema Komba.
Kwa upande wake Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa MNH-Mloganzila, Dkt. Julieth Magandi amewashukuru kwa kushukuru baada ya kupatiwa matibabu na kuwasihi wakawe mabalozi wazuri wa hospitali kwani huduma bora zipo.
“Tunawashukuru kwa kurudi kushukuru kwa huduma mliyopatiwa hospitalini hapa, nawasihi mkawe mabalozi wazuri wa hospitali hii kwani huduma bora zipo” amesema Dkt. Magandi.