Baadhi ya wanafunzi waliofutiwa matokeo ya Mitihani ya kumaliza Darasa la Saba mwaka huu katika Shule ya Msingi Muungano wilayani Tunduru mkoani Ruvuma wakiwa na mabango yenye ujumbe wa kumuomba Rais Dkt John Magufuri kuwasaidia kupatiwa matokeo yao au waruhusiwe tena kusoma katika shule za Serikali ,Watoto hao wamesema wako tayari kurudia darasa au kushushwa madarasa ya chini ili waendelea na masomo kwani iwapo watabaki nyumbani kuna hatari kubwa ya kushindwa kutimiza ndoto zao.
Picha na Mpiga Picha Wetu.
…………………………………………………………………………………….
Na Mwandishi Wetu,Tunduru
WANAFUNZI zaidi ya 100 waliofutiwa matokeo ya mtihani wa kumaliza Darasa la saba mwaka 2019 katika shule ya Msingi Muungano wilaya ya Tunduru, wamemuomba Rais Dkt John Magufuri kuwasaidia kupatiwa matokeo ya mitihani hiyo ili waweze kuendelea na elimu ya sekondari katika muhula wa masomo wa 2020 ulioanza tangu Januari sita mwaka huu.
Wakizungumza kwa masikitiko makubwa huku wengine wakiangua kilio watoto hao wamesema,kitendo cha kufutwa na kuzuiwa matokeo ya mitihani yao kimewaumiza sana kwani kimekatisha ndoto za maisha yao.
Watoto hao wenye umri kati ya miaka kumi na moja hadi kumi na mbili walisema, katika muda wa miaka saba walipokuwa shule walijitahidi kusoma kwa bidii ili waweze kufanya vizuri katika mitihani ya mwisho itakayowawezesha kuendelea na elimu ya sekondari jambo ambalo kwa sasa limeishia njiani.
Wakizungumza kwa niaba ya wenzao Bilal Abdala,Rehema Adam walisema, sababu za kuzuiliwa matokeo yao hawazifahamu na kumuomba Rais Dkt Magufuri na Waziri wa Elimu Profesa Joyce Ndalichako kufanya uchunguzi wa kina juu ya sakata hilo.
Bilal Abdala alisema, tukio hilo limewaumiza sana kwani kwa muda wote wa miaka saba waliyosoma dhamira yao ni kufanya vizuri Darasani ili wapate nafasi ya kuendelea na masomo ya elimu ya sekondari na vyuo vikuu,lakini wanaona kama ndoto zao zimekatishwa njiani.
Aidha alisema, mpaka sasa bado hawajapata taarifa sahihi sababu ya kutopata matokeo ya mitihani yao, hivyo kuiomba Serikali kuwaangalia kwa jicho la huruma kwani bado dhamira yao kuendelea na shule.
Rehema Adam amemuomba Rais wa wanyonge Dkt John Magufuri, kuwafungulia njia ya ndoto zao kwa vile bado watoto wadogo wanaohitaji kusoma ili watakapomaliza waweze kuzisaidia familia zao,jamii na nchi kwa jumla.
Alisema, kuzuiwa kwa matokeo ya mitihani yake kumemaliza ndoto zake za kuwa Daktari na kiongozi Bora ambaye alitamani sana kuona anawatumikia Watanzania wenzake katika nafasi mbalimbali za uongozi.
“ sisi bado watoto wadogo tunaohitaji sana kuendelea na masomo,tunamuomba Rais wetu Magufuri atusaidie ili tuweze kutimiza ndoto zetu,mpaka sasa hatufahamu sababu za kufutwa kwa matokeo ya mitihani yetu”alisema Adam.
Wazazi wa watoto hao wakiongozwa na Adam Msuya walisema, baada ya mitihani ya Darasa la saba watoto wao walipewa vikaratasi vilivyoandikwa herefi SW ambazo wao hawakufahamu maana yake na walipo fuatilia kwa afisa elimu wa wilaya walielezwa kuwa watoto wao wamefanya udanganyifu wakati wa mitihani.
Msuya alisema, walielezwa kuwa watoto wao wakati wa mitihani hiyo waliangaliziana majibu ya maswali jambo alililosema, haliwezekani kwa idadi kubwa ya watoto kuangaliziana majibu ya mitihani kwa wakati mmoja.
Kwa mujibu wa Msuya ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ya wazazi iliyoundwa kufuatilia sakata hilo alisema, walikwenda hadi kwa Mkuu wa wilaya ambaye naye aliwapa majibu kuwa matokeo ya watoto wao yamefutwa kutokana na udanganyifu na kuwataka wazazi kuwatafutia vyuo vya ufundi watoto wao kwani wamepoteza sifa ya kuendelea na masomo ya sekondari katika shule za serikali.
Msuya amemuomba Rais Dkt John Magufuri kuwasaidia wazazi na watoto hao kumaliza sakata hilo ambalo linaweza kuongeza idadi ya watu wasiokuwa na ajira na waharifu katika nchi hii.
Aidha amemuomba Rais Magufuri kuwachukulia hatua baadhi ya watendaji wa idara ya elimu walio husika katika sakata hilo ambalo amelitaja ni uonevu kwa watoto wao.
Mzazi mwingine Happines Shenga alisema, wao kama wazazi wameumizwa sana na sakata hilo hasa ikizingatia kuwa umri wa watoto wao ni mdogo na hawezi kufanya kazi yoyote ya kujiingizia kipato.
Amemtaka Waziri wa elimu Profesa Joyce Ndalichako kuunda tume huru ambayo itafuatilia tatizo hilo na kuwachukulia hatua kali wale wote ambao wamesababisha kutokea kwa sakata hilo.
Kwa upande wake Afisa Elimu ya msingi wilaya ya Tunduru Anderson Mwalongo alieleza kuwa, tatizo hilo halikuwa katika shule ya Muungano tu bali lilitokea katika shule nyingine ya Kitanda na Mchangani.
Alisema, suala la kufutwa matokeo ya wanafunzi hao sio la Halmashauri ya wilaya bali Bodi ya Baraza la mitihani ndilo linahusika juu ya sakata hilo ambapo liliunda Tume maalum ambayo ilijiridhisha kuwepo kwa kasoro hilo kwa baadhi ya watoto kuangaliziana majibu ya mitihani waliyopewa.
Mwalongo alisema, wao kama Halmashauri walichukua hatua kwa walimu 11 ambao walikuwa wasimamizi wa vyumba vya mitihani na tayari wameshafikishwa katika Tume ya Utumishi ya Walimu kwa ajili ya hatua za kinidhamu sambamba na kuwashusha madaraka walimu wakuu wa shule hizo tatu.
Hata hivyo amewashauri wazazi kuwa, vijana wao wana nafasi kubwa ya kusoma kupitia nje ya mfumo usio rasmi ambao utamwezesha mwanafunzi kujiendeleza na kama atafanya vizuri kupitia mfumo huo, anaweza kujiunga na shule za sekondari za Serikali kwa kidato cha tatu,nne na kuendelea