Walimu wakuu washule mbalimbali za msingi katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni wakikagua madarasa yanayojengwa wakati wa ziara na Afisa Elimu Msingi wa Halmashauri hiyo Kiduma Mageni.
Muonekano wa madarasa yanayojengwa.
Muonekano wa madarasa yaliyojengwa na kukaribia kutumika kwa wanafunzi wa shule za msingi katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni.
Mmoja wa walimu wakuu waliokuwa katika ziara hiyo, akieleza mbele ya walimu, Afisa Elimu mwenendo wa ujenzi wa madarasa katika shule yake ulipofikia.
***********************************
Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imetumia kiasi cha shilingi Bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi na ukaratabati wa vyumba 107 vya madarasa pamoja na matundu ya choo 157 kwa wanafunzi wa shule za msingi zilizopo katika Halmashauri hiyo.
Hayo yamebainisha na Afisa elimu msingi wa Halmashauri hiyo Kiduma Mageni wakati wa ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya shule iliyokuwa na lengo la kuona maendeleo ya miradi hiyo ambayo inatekelezwa kwa kutumia Force Account.
Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa ziara hiyo, Ndugu Mageni alisema kuwa katika fedha hizo zilizotumika kujenga na kukarabati vyumba hivyo vya madarasa pamoja na matundu ya choo, shilingi milioni 771, 520,000 zinatokana na makusanyo ya ndani, shilingi milioni 455,140,000 ni pesa kutoka serikali kuu kupitia mpango wa EP4R.
Aidha Mageni ameongeza kuwa katika fedha hizo pia kiasi cha shilingi milioni 210, 004, 726 ni pesa kutoka mpango wa madarasa 100 ya Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Daniel Chongolo, na kiasi cha shilingi milioni 4, 140,000 nipesa zinazotokana na nguvu za wananchi.
Sambamba na hivyo, ndugu Mageni amebainisha madarasa yaliyojengwa ni 58, yaliyokarabatiwa ni 42 na kwamba kwa vyumba vilivyokarabatiwa vimeanza kutumika na wanafunzi huku vile vinavyojengwa vikiwa vimekamilika kwa asilimia 95.
Mageni amesema Halmashauri ya Kinondoni kupitia Mkurugenzi Aron Kagurumjuli pamoja na Mkuu wa Wilaya Mhe. Daniel Chongolo wamekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa inajenga na kukarabati madarasa hayo ili wanafunzi waweze kusoma katika mazingira mazuri.
Ameongeza kuwa Serikali ya awamu ya tano inayo ongozwa na Rais Dk. John Pombe Magufuli inatoa elimu bure na kwamba viongozi hao Mkurugenzi Kagurumjuli na Mkuuwa Wilaya Chongolo wanaitekeleza kikamilifu sera hiyo.
“ Niwapongeze sana kwa kazi nzuri wanayoifanya, tumejionea wenyewe wanafunzi wanakaa kwenye majengo mazuri,ya kisasa ,mengine bado yapo kwenye hatua ya mwisho kukamilika na muda sio mrefu yatakabidhiwa ili watoto wetu wa anze kuyatumia.
“Nampongeza sana Mhe. Chongolo, Kagurumjuli na timu yake yote wanafanya kazi kubwa, inaonekana, Rais wetu Dk. Magufuli ametoa elimu bure na sisi tunaitekeleza, nasio kwamba tunaishia hapa, bado tutaendelea kutekeleza zaidi na zaidi ili watoto wetu wasome kwenye majengo safi” alisema Mageni.
Mageni amesema ameridhishwa na ujenzi, ukarabati wa majengo hayo na hivyo kuwataka walimu hao kuwa wasimamizi wazuri wa miundombinu hiyo.
Kwa upande wa mwalimu hao waliokuwa katika ziara hiyo wamempongeza Mkurugenzi Kagurumli kwa kuwezesha ujenzi wa madarasa hayo na kwamba wanafunzi watasoma kwa nafasi.
Mmoja wa walimu hao ambaye ni Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Mwenge, Janeth Mlenge alisema kuwa elimu bure inayotolewa na Rais Dk.Magufuli imetoa hamasa kwa wazazi na hivyo kuwepo kwa idadi kubwa ya wanafunzi wanaosoma.
Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Nyakasanga amesema kuwa kupitia mradi huo katika shule yake amejengewa vyumba nane vya madarasa ofisi ya mwalimu mkuu pamoja na matundu 13 ya choo na hivyo kumpongeza Mkurugenzi Kagurumjuli,Mhe. Chongolo kwa kuwapatia majengo hayo.
Hata hivyo walimu hao wameonyesha kufurahishwa na huduma hiyo ya kujengewa madarasa katika shule zao, sambamba na kukarabatiwa na kusema serikali kupitia Halmashauri ya Kinondoni inatekeleza vema sera ya Elimu bila malipo.