Akipanda mti kuashiria uzinduzi kulia kwake ni mmiliki wa shamba Bi Desderia Komba ambaye amehamasika kulima zao hilo kutokana na maboresho ya serilali ya awamu ya tano..
Ofisa kilimo wa kata ya Kingerikiti Wilayani hapa Richard Katale (Mwenye kanzu) ambaye pia ni mkaguzi wa zao la kahawa wilayani Nyasa, akitoa mafunzo kwa wakulima wa zao la kahawa juu ya upandaji miche mipya, ya kahawa aina ya Compact kabla ya kuwagawia wakulima waweze kupanda miche hiyo hivi karibuni katika Kata ya Kingerikiti Wilayani Nyasa.
Mkuu wa Idara ya Kilimo, Umwagiliaji na ushirika Menance Ndomba, (mwenye shati jeupe) aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Bi Isabela chilumba, akigawa miche ya kahawa katika uzinduzi wa ugawaji miche mipya ya Kahawa, aina ya Compact kwa wananchi wa Wilaya ya Nyasa, uzinduzi uliofanyika hivi karibuni katika kijiji cha Kingerikiti na Kata ya Kingerikiti Wilayani Nyasa.
…………………………………………………………………………………………………
Wakulima wa zao la kahawa Wilayani Nyasa, kwa kushirikiana na Vyama vya Msingi vya mazao na watu binafsi, wamezalisha miche ya kahawa 262,500 kwa msimu wa kilimo 2019/2020 ili kuongeza uzalishaji wa zao la kahawa na kukuza uchumi wa wananchi.
hayo yamesemwa na wakulima wa zao la kahawa katika Risala yao, kwa mgeni Rasmi Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Bi Isabela O.Chilumba, wakati akizindua ugawaji wa miche mipya ya kahawa aina ya “Compact” Uzinduzi uliofanyika Hivi karibuni, katika Kijiji cha Kingerikiti Kata ya Kingerikiti Wilayani hapa.
Wakulima hao wamefafanua kuwa, wamelazimika kuongeza uzalishaji wa zao la kahawa ikiwa ni pamoja, na utekelezaji wa Agizo la Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Cassim Majaliwa aliyezitaka kili Halmashauri Nchini kuzalisha miche ya kahawa zaidi ya laki mbili.
Waliongeza kuwa Vyama saba vya Ushirika wa mazao vimezalisha miche hiyo na tayari kwa kugawa kwa wananchi kwa mchanganganuo ufuatao Nambawala AMCOS (10250), Kingerikiti AMCOS miche( 37,705), Tingi AMCOS (4,300) LIPO AMCOS MICHE (40,000), Mapendo AMCOS Miche (36,000) na Luhangarasi AMCOS 9890.
Pia wakulima hao walikipongeza kituo cha utafiti cha Ugano (TACRI) kwa kuwagawia bure miche kahawa 18,200 aina ya compact, ambayo wameigawa kwa wakulima ambao wanauhitaji wa miche hiyo.
Akitoa maelekezo ya upandaji wa miche hiyo kwa wakulima wa zao la kahawa, Ofisa kilimo wa Kata ya Kingerikiti ambaye pia ni Mkaguzi wa zao la Kahawa Bw.Richard Katale, aliwataka wakulima, kulihudumia vizuri, kwa kupanda kwa nafasi ya Meta mbili na kwa Hekari moja watapanda meche mia sita.
Aliongeza kuwa sifa za mche wa compact unazaa mapema na unavumilia ukame. Alikawataka wananchi kupanda kwa maelekezo aliyoyatoa, ili kufikia uzalishaji wenye tija kwa kuwa Serikali imedhamiria kuboresha maisha ya wakulima wa zao la Kahawa.
Aidha wakulima hao, waliipongeza Serikali ya awamu ya tano kwa kufanya maboresho mbalimbali ya zao la kahawa, na kuwaletea mnada wa kahawa katika Wilaya ya Mbinga na kuwapunguzia usumbufu kwa kuwa awali walikuwa wakienda moshi kufanyia mnada.
“kwa kweli awamu hii tunaona jinsi gani Serikali inatujali wakulima, kwa kuwa tunapewa mafunzo ya kulima kahawa, lakini pia kitendo cha kutupa miche ya ya kahawa bure , Serikali imetusaidia sana. Nimejaribu kupanda na nimeona ni mbegu nzuri inayotoa mavuno mengi kwa muda mfupi ukilinganisha na kahawa tuliyozoea kupanda awali”. Alisema Bonus mapunda mkulima wa zao la kahawa kutoka katika kijijii cha kingerikiti.
Akizungumza na wakulima wa zao la Kahawa Wilayani hapa, Mkuu wa Idara ya Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika Bw.Menance Ndomba aliyemwakilisha mkuu wa Wilaya ya Nyasa Bi,Isabela Chilumba,Aliwapongeza wakulima wa Zao la kahawa Wilayani Nyasa, kwa juhudi wanazozifanya za kulima na kutunza zao hilo na kuinua mapato ya Halmashauri na kuwa na kipato bora cha Familia na kuchangia maendeleo mbalimbali katika maeneo yao.
Aidha aliwataka kuendelea kuongeza uzalishaji wa zao la Kahawa kwa kuwa , Wilaya ya Nyasa ina Fursa ya mashamba makubwa, kwa mujibu wa Utafiti uliofanyika hivi karibuni na “CAFE Afrika” katika Wilaya ya Mbinga na Nyasa Wilaya ya Nyasa ina fursa kubwa ya kupanua mashamba ya kahawa ukilinganisha na Wilaya ya Mbinga.
“nachukua fursa hii kuwapongeza sana wakulima wa zao la kahawa Wilayani Nyasa, kwa kazi nzuri mnayoifanya ya kujituma kulima na kuzalisha zao hili la kahawa ambalo linatupa faida kubwa sana katika Halmashauri yetu kama vile ,mapato ya ndani na mnachangia maendeleo mbalimbali katika maeneo yenu.Serikali ipo pamoja nanyi na itatatua changamoto mbalimbali mtakazokutana nazo katika shughuli zenu na kuhakikisha Miundombinu inajengwa. Alisema ndomba.
Wilaya ya Nyasa ipo katika Mkakati wa kuongeza uzalishaji wa mazao ya biashara ya Kahawa,kakao, na korosho ili kukuza uchumi wa kipato cha mwananchi mmoja mmoja na Wilaya kwa ujumla.