Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Arch. Elius Mwakalinga, akizungumza na Mameneja wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), kutoka mikoa mbalimbali nchini katika kikao kilichowakutanisha mameneja hao kujadili tathmini ya utendaji kazi wa Wakala huo, jijini Dodoma. Kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Wakala huo, Daudi Kondoro.
Mameneja wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), kutoka mikoa mbalimbali nchini wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Arch. Elius Mwakalinga, katika kikao kilichowakutanisha mameneja hao kujadili tathmini ya utendaji kazi wa Wakala huo, jijini Dodoma.
Kaimu Meneja wa Wakala wa Majengo (TBA), mkoa wa Rukwa, Arch. David Luoga na Kaimu Meneja wa TBA mkoa wa Singida, Mhandisi Rebecca Kimambo, wakitoa maoni yao kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Arch. Elius Mwakalinga, katika kikao kilichowakutanisha mameneja hao kujadili tathmini ya utendaji kazi wa Wakala huo, jijini Dodoma.
………………………………………………………………………………..
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Arch. Elius Mwakalinga, ameutaka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), kujitathmini na kubadilika katika utekelezaji wa miradi yake ili kuondosha taswira mbaya iliyojengeka katika jamii dhidi yao.
Akizungumza katika kikao cha kujadili tathmini ya utendaji kazi wa Wakala huo kilichofanyika jijini Dodoma, Katibu Mkuu huyo amesema kuwa zoezi hilo la kujitathmini litasaidia kubaini kasoro walizonazo za utoaji huduma kwa wateja wao na kuzitafutia ufumbuzi na hivyo kusaidia kujenga tena taswira nzuri ya Wakala huo.
“Nataka mtumie kikao hiki kuangalia na kujadili changamoto zinazowapelekea msifanye vizuri kwa sasa na mzipatie ufumbuzi, nadhani mnayaona na kuyasikia yanayosemwa na wateja wenu, malalamiko ni mengi na kiukweli hayaridhishi”, amesema Katibu Mkuu Mwakalinga.
Aidha, Mwakalinga amefafanua kuwa, Wakala huo umekuwa ukilalamikiwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo la uandaaji wa makisio ya gharama za ujenzi (BOQ), usanifu wa michoro na kutokumaliza miradi kwa wakati ambapo amesisitiza Wakala huo kuyaangalia kwa makini maeneo hayo ili kumaliza sintofahamu kwa wateja wao.
“TBA mnaaminika kwa suala la ubora na weledi, ila kuna baadhi ya maeneo ambayo hamfanyi vizuri, naomba kuanzia sasa mbadilike ili wateja wenu waendelee kuwaamini”, amesisitiza Mwakalinga.
Mwakalinga amewataka TBA kushirikiana na kutojihusisha na majungu kwani hayana tija katika kuleta maendeleo ya Wakala huo na Taifa kwa ujumla.
Katibu Mkuu Mwakalinga, ameongeza kuwa hawatawavumilia wale wanaodaiwa kodi na Wakala huo kwani miradi mingi inashindwa kutekelezwa kutokana na madeni ambayo Wakala wanadai kwa wateja wao.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Daudi Kondoro, amemhakikishia Katibu Mkuu huyo kutekeleza maelekezo aliyowapa na kutatua changamoto walizonazo.
“Naomba nikuhakikishie Katibu Mkuu kuwa mbali na kuwepo kwa changamoto ya mtiririko wa fedha kutoka kwa washtiri, wakala utajitahidi kufuatilia madeni na kuhakikisha tunalipwa kwa wakati ili kusaidia kutekeleza miradi mingine”, amesema Kondoro.
Ameahidi kuzifanyia kazi changamoto za ndani walizonazo kama vile upungufu wa watumishi na suala la uandaaji wa makisio ya gharama za ujenzi ambapo amesema kuwa atawasilisha ripoti ya majibu ya changamoto hizo kwake mara baada ya kikao hicho kumalizika.