Naibu Katibu Mkuu Dkt. Dorothy Gwajima akizungumza na Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Dkt. Angelina Lutambi, muda mfupi baada yakuwasili.
Naibu Katibu Mkuu Dkt. Dorothy Gwajima akitoa somo kwa timu za Afya za Mkoa wa Singida.
Bibi Mary Shedrack mtaalam kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, akitoa mchango wake mbele ya timu za Afya ambazo hazipo kwenye picha
Katibu Tawala Mkoa wa Singinda Dkt. Angelina Lutambi, akimkabidhi zana za utendaji kazi Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singiada mara baada ya Semina ya utendaji kazi iliyoendeshwa na Naibu Katibu Mkuu.
Naibu Katibu Mkuu Dkt. Dorothy Gwajima akitoa somo kwa timu za Afya za Mkoa wa Singida.
……………….
Na. Atley Kuni- SINGIDA.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI, anayeshughulikia masuala ya Afya Dkt. Dorothy Gwajima, ametumia saa 2 na dakika 56 kuwafunda na kuwakumbusha watumishi wa kada ya afya juu ya majukumu yao ya msingi na kuwahimiza kuyafuata kwa kuyawekea mipango halisi.
Dkt. Gwajima amefanya hayo mwishoni mwa juma katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida alipokutana na timu za uratibu Afya za Wilaya zote za Mkoa huo wakiongozwa na timu ya Afya ya Mkoa.
Akitoa somo katika kikaokazi hicho ambacho pia kilihudhuriwa na Katibu Tawala wa Mkoa huo Dkt. Angelina Lutambi, Dkt. Gwajima alisema, changamoto kubwa inayowakabili watumishi wengi ni kushindwa kupanga mpango mzuri wa kutekeleza kikamilifu majukumu yao ya ajira kwa vigezo stahiki. Alisema, utekelezaji unaofanyika nikwa mazoea lakini sio kwakufuata uhalisia kwa takwimu bayana.
Aliwataka Viongozi na waratibu hao wa afya kuimarisha mifumo ya utekelezaji wa majukumu kwa kuhakikisha kwanza kila mtumishi amepewa majukumu yake na kueleweshwa ipasavyo, kisha kuongozwa kwa kuandaa mpango kazi wake wenye vigezo na siyo jumla jumla tu kwani bila kufanya hivyo watumishi wengi hujikuta wanatekeleza majukumu ya mazoea na kwa mifumo ya mazoea.
Kuhusu suala la majukumu yanayohusu utawala wa masuala ya afya Dkt Gwajima alisema, hilo ni suala mtambuka linalohusu wataalamu wengi wakiwemo maafisa utumishi, maafisa manunuzi, wakaguzi wa ndani, waajiri na wengine kutoka idara mbalimbali zisizoangukia sekta ya afya kitaaluma. Dkt. Gwajima alisema iwapo wataalamu hawa hawatawajibika kikamilifu na kwa wakati basi nao wanaweza kuchangia ufanisi wa utekelezaji majukumu ya afya kushuka viwango.
Akitoa mfano wa uhusiano wa Idara zisizo za taaluma ya sekta ya afya alisema “je dokezo la kuomba utekelezaji wa shughuli za afya huchukua muda gani kufanyiwa kazi na afisa manunuzi, afisa utumishi, afisa fedha na wataalamu wengine?” Alihoji Dkt. Gwajima.
Jinsi gani Afisa Utumishi anaona umuhimu wa kuchambua uwingi wa kazi baina ya watumishi na kuwafanyia mgawanyo upya? Au Mkaguzi wa ndani anasimamia vipi masula ya ukaguzi wa stoo zetu za mali mbalimbali iwapo mifumo ikp vizuri ikiwemo dawa na uwepo wa kumbukumbu za mali zilizopo kwenye vituo kwa ujumla?” alizidi kuhoji Dkt. Gwajima.
Aidha alisema, katika hili la utawala lazima kila mtu kwa nafasi yake asimame kidete ili sekta hii inayochangia katika safari ya kwenda uchumi wa kati iweze kuwa ma utayari wakati wote katika kuhakikisha abiria wote wako katika afya njema kwa ajili ya kushiriki kikamilifu shughuli za maendeleo.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa huo, Dkt. Angelina Lutambi, alisema tatizo kubwa lililopo kwa sasa ni kwa baadhi ya watumishi kutokuwa na ubunifu wa maarifa na kufanya kazi kwa mazoea.
“Utakuta mtu ni Mkuu wa Idara lakini ukimuuliza umetelekeza majukumu gani hajui, anakwambia hujanipatia jambo la kufanyia kazi, wakati mtu huyo ana muongozo wa majukumu yake.” Alisema Dkt. Lutambi na kuongeza kuwa, kuanzia sasa atayasimamia yote ambayo Naibu Katibu Mkuu amewaelekeza watendaji wa mkoa huo na kwamba, hata yeye tayari alishaona hizo changamoto na sasa atahitaji kupata taarifa ya kila wiki kupitia kwa Mganga Mkuu wa Mkoa kuhusu muelekeo wa masuala ya Afya katika Mkoa.
Kwa upande wake Mlezi wa Mkoa wa Singida katika masuala ya afya, kutoka OR-TAMISEMI, Bibi Mary Shedrack alisema, ili sekta iweze kufanikiwa lazima kuzingatia vigezo vitakavyo waongoza kwa kila mmoja kuvitatumika na kupima kwa kila robo.
Ziara ya Dkt. Dorothy Gwajima ni muendelezo wa ziara za kikazi anazo zifanya katika kufatilia masuala mbali mbali ya afya nchini na katika ziara hii imemchukua siku mbili katika Mkoa wa Singida kwa ajili yakufatilia hali ya utoaji huduma za afya na vilelvile kuzungumza na timu za uratibu za afya za Wilaya za Mkoa huo.