Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, (aliyesimama) akizungumza katika kikao cha ndani na wafanyakazi wa TANESCO, REA, wakandarasi pamoja na viongozi wa wilaya ya Nyang’hwale alipofika kufanya kazi ya kukagua maendeleo ya usambazaji umeme wilayani hapo, kulia ni Mkuu wa Wilaya hiyo Hamim Gwiyama na Mbunge wa jimbo la Nyang’hwale, Husein Nassoro Amir.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, (katikati) akitoa maelekezo kwa watendaji wa TANESCO kuharakisha ufungaji wa mashineumba hiyo na kuwashwa umeme katika mgodi wa Nyamigoro haraka.
Wanafunzi wa shule ya msingi Bukwimba wilayani Nyang’hwale mkoani Geita wakifurahia kuwashwa kwa umeme katika shule yao iliyoanzishwa mwaka 1958 ikiwa ni takribani miaka 62 bila kuwa na umeme.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, (katikati) akikata utepe na kuwasha umeme katika mgodi na mtambo ya kuchenjua madini ya dhahabu wa Mwabomba wilayani Kahama mkoani Shinyanga.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, akioneshwa jinsi umeme unavyosaidia kurahisisha kazi ya kuchenjua dhahabu kwa kutumia teknolojia ya kisasa katika mgodi wa Mwabomba wilayani Kahama mkoani Shinyanga.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, (kulia) akipitishwa na mmiliki mgodi na mtambo wa uchenjuaji dhahabu wa Mwabomba (kushoto) katika sehemu ya mtambo huo unatumia umeme kuendesha shughuli za
uchenjuji dhahabu kwa kutumia teknolojia ya kisasa ambayo ni rafiki kwa binadamu na mazingira.
**********************************
Zuena Msuya, Shinyanga
Imeelezwa kuwa dhamira ya Serikali katika kuwainua wachimbaji wadogo kwa kuwaunganishia huduma ya umeme katika migodi na mitambo ya kuchenjulia dhahabu ili kuwapunguzia gharama za uendeshaji na kupata
faida kubwa zaidi.
Dhamira hiyo ilidhihirishwa wazi na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, Januari 24, 2020, wakati akiwasha umeme katika mgodi na mtambo wa kuchenjua dhahabu wa 136 kuwashiwa umeme nchi nzima uliopo katika Kijiji cha Mwabomba wilayani Kahama mkoani Shinyanga.
Dkt. Kalemani alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano kupitia sera ya uchumi wa viwanda imedhamiria kuwainua na kuwathamini zaidi wachimbaji wadogo kwa kuhakikisha inawaunganishia umeme wa bei nafuu wale wote wenye migodi na mitambo ya kuchenjua dhahabu, ili umeme huo uwarahisishie shughuli za uendeshaji na kuinua vipato vyao.
Alisema umeme katika sehemu za migodi utampunguzia mchimbaji mdogo gharama za uendeshaji na kupata faida ambayo pia atalipa kodi na tozo mbalimbali za serikali bila vikwazo na kuiongezea serikali mapato.
"Tutahakisha migodi na mitambo yote ya kichenjua dhahabu au madini ya aina yeyote ile hapa nchini inaunganishiwa umeme, hii itasaidia pia kuwa
wachimbaji wa kisasa zaidi kwa kutumia teknolojia bora ambazo hazitaruhusu hata chembe ya madini yao kupotea, na teknolojia hizo ni rafiki kwa binadamu na mazingira kwa jumla, bila umeme technolojia nyingine hawataweza kuzitumia", alisema Dkt. Kalemani.
Akizungumzia usambazaji wa umeme vijijini, Waziri aliliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuunganisha kata zote 20 ambazo hazijaunganishwa na umeme hadi kufikia mwezi Aprili mwaka huu katika
Wilaya ya Kahama.
Alieleza kuwa wananchi hawataki kusikia habari ya aina yeyote juu ya umeme, zaidi ya kuona unawaka ndani ya majumba yao na hakuna sababu ya msingi ya kuwafanya wananchi hao wakose umeme kwa kuwa tayari
fedha zipo na vifaa vyote vinapatikana hapa nchini na watalaamu wa kazi hiyo wapo.
Mapema akiwa katika ziara hiyo wilayani Nyang'hwale, mkoani Geita, Dkt. Kalemani, aliiagiza (TANESCO) kukamilisha ufungaji wa mashineumba
(Transfoma) na kuwasha umeme katika mgodi wa Nyamigongo ambao hutumia zaidi ya shilingi milioni 120 kwa mwezi ikiwa ni gharama za kununua Mafuta ya kuendesha shughuli za Uzalishaji tofauti na umeme
angetumia takribani milioni 80.
Aliwaeleza TANESCO kuwa, mashineumba watakayofunga si kwamba itamnufaisha mwekezaji huyo pekee, bali zaidi ya vijiji 20 vinavyomzunguka vitatumia mashineumba hiyo kuwasambazia umeme.
Aidha, shirika hilo litapata faida kubwa itakayowawezesha kuendelea kusambaza umeme na kuboresha miundombinu iliyochakaa ama kuharibika.
Kwa upande wao wamiliki wa migodi hiyo, wameishukuru serikali kwa kuwathamini wachimbaji wadogo ambao walikuwa kama wametelekezwa katika kutatuliwa matatizo na changamoto mbalimbali zinazowakabili
ikiwamo kuboreshwa kwa shughuli zao za uchimbani kwa manufaa zaidi.
Vilevile, akiwa Wilayani, Nyang'hwale Waziri huo wa Nishati, aliwasha umeme katika shule ya msingi iliyoanzishwa mwaka 1958 takribani miaka 62.
Aidha, alitembelea eneo linalojengwa Makao Makuu ya Wilaya ya Nyang’hwale, Hospitali na majengo mengine ya serikali na kuagiza TANESCO kufunga mashineumba yenye uwezo mkubwa katika eneo hilo ili iharakishe shunguli za kiutendaji.
Pia, alimuagiza mkandarasi anayetekeleza mradi wa usambazaji umeme vijijini katika wilaya hiyo, kuongeza kasi ya kuunganishia umeme mara tuu baada wateja kuliolipia na kuongeza kasi ya usambazaji umeme katika
vijijini wanavyotekeleza mradi huo na kuwasha vijiji vitatu kila wiki.
Vilevile, alimtaka kuondoa nguzo zilizorundikwa sehemu moja kwa muda mrefu na kuzisambaza katika maeneo mbalimbali zinapohitajika na endapo ni mbovu basi azirudishe kwa walikozinunua ili wapatiwe nguzo zingine
kulinagana na makubaliano yanavyoelekeza.
Kwa upande wake, mkuu wa wilaya hiyo, Hamim Gwiyama alimuhakikishia Waziri huo kuwa kabla ya majengo hayo kukamilika watalipia gharama za uunganishaji umeme katika majengo ili umeme huo pia usaidie shughuli za
umaliziaji ujenzi wa majengo hayo.
Vilevile, wataendelea kulipia Taasisi za Umma kama shule, vituo vya Afya na Taasisi za Dini zilizopo katika maeneo yao ili ziunganishiwe umeme.