Na. Alex Sonna,Dodoma
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe Selemani Jafo amekerwa na uchafu wa mazingira uliopo katika soko la Sabasaba jijini Dodoma na kumuagiza Mkurugenzi wa Jiji hilo kuhakikisha ujenzi wa soko hilo unaanza kabla ya kuisha kwa Bunge la bajeti.
Mhe Jafo amesema ni jambo la aibu kwa Jiji la Dodoma linaloongoza kwa kukusanya mapato takribani Bilioni 71 kuwa na soko lenye mazingira machafu yanayohatarisha maisha ya wananchi.
Kauli hiyo ameitoa leo mara baada ya kufanya ziara yake ya kikazi na kukagua ujenzi wa Hospitali ya Uhuru iliyopo wilayani Chamwino kabla ya kupita kujionea hali ilivyo kipindi hichi cha mvua kwenye soko hilo la Sabasaba.
“Jiji la Dodoma halina mashaka katika ukusanyaji wa mapato, na najua mnafanya mambo makubwa na mazuri lakini kwa hili hapana sijaridhishwa kabisa na hali ya soko, hili ni jambo pana la wananchi ni vyema likafanyiwa kazi kwa haraka” amesema Mhe. Jafo
Aidha amesema kuwa wafanyabishara hawa ni wapiga kura wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli, hivyo wanatakiwa kufanya biashara katika mazingira mazuri na si katika mazingira haya, wanatakiwa wafanye biashara katika mazingira masafi .
“Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma sijafurahishwa na hali ya uchafu unaoendelea katika soko hili, uchafu huu unahatarisha afya za wafanyabishara na wananchi kwa ujumla, nakuagiza kuhakikisha Soko hili linafanyiwa ukarabati” Amesisitiza Mhe Jafo
Aidha, Mhe. Jafo ameutaka uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kuhakikisha wanasimamia usafi na kuhakikisha mitaro inasafishwa ili kulinda afya na usalama wa wafanyabishara na wananchi kwa ujumla.
Awali Mhe Jafo alitembelea ujenzi wa Hospitali ya Uhuru inayojengwaWilaya ya Chamwino mkoani Dodoma na kumuagiza mkandarasi anaesimamia ujenzi huo kuhakikisha anajenga mchana na usiku ili kumaliza ujenzi huo mapema na wananchi waanze kutibiwa.
” Hii Hospitali Mhe Rais alitoa fedha za Uhuru ili zijenge hapa wananchi waweze kupata matibabu. Nafahamu kumekua na mvua kukawa na changamoto lakini tayari mvua zimepungua hivyo ujenzi uendelee usiku Na mchana.
Nimewaelekeza Suma JKT ambao ndio wanasimamia ujenzi huu kufunga taa kubwa hapa ili ujenzi uendelee mchana na usiku lengo tuweze kumaliza mapema na wananchi wetu wafurahie matunda ya serikali yao,” Amesema Mhe Jafo.
Ujenzi wa Hospitali ya Uhuru ulianza rasmi Oktoba 26, 2019 na Novemba 22 Mhe Rais Magufuli aliweka jiwe la msingi la ujenzi ambalo Novemba 23 alitoa maelekezo ya kuhamisha ujenzi huo kutoka kitongoji cha Maduma kwenda eneo la Buigiri, Chamwino ambapo sasa ujenzi huo unatarajia kukamilika Mei 25 mwaka huu.