Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe.Dkt.Harrison Mwakyembe akizungumza na wadau wa tasnia ya habari mkoani Kilimanjaro (hawapo pichani)
katika kikao cha kuimarisha utendaji wa wanahabari pamoja na kutatua changamoto za tasnia hiyo alipokua katika ziara ya kukagua usikivu wa TBC mkoani hapo Januari 24,2020.Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Moshi Mhe.Kippi Warioba na kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania Dkt.Ayoub Ryoba.
Baadhi ya wanahabari wa Mkoa wa Kilimanjaro wakiwasilisha hoja zao kwa Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe.Dkt.Harrison Mwakyembe(hayupo pichani) katika kikao na wanatasnia hao kilichofanyika Januari 24,2020.
Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe.Dkt.Harrison Mwakyembe akiwa katika picha ya pamoja na wadau wa tasnia ya habari mkoani Kilimanjaro mara baada ya kumaliza kikao cha kuimarisha utendaji wa wanahabari pamoja na kutatua changamoto za tasnia hiyo alipokua katika ziara ya kukagua usikivu wa TBC mkoani
hapo Januari 24,2020.
**********************************
Na Mwandishi wetu -Kilimanjaro
Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo amesema kuwa ipo haja kwa Vyuo vyote vinavyofundisha taaluma ya habari kufundisha somo la historia ya Ukombozi wa
bara la Afrika ili kuzalisha wanahabari wenye uelewa wa kutosha kuhusu Bara hili.
Mhe.Mwakyembe ameyasema hayo jana Mkoani Kilimanjaro alipokua akizungumza na wanahabari wa Mkoa huo ambapo amesema kuwa wanahabari wanapaswa kuwa na uelewa kuhusu Bara la Afrika ili waweze kuandika mambo mazuri kuhusu Afrika.
“Msipojua historia ya Bara letu la Afrika mtaendelea kushabikia taarifa zinazotolewa na taasisi za watu wa nje bila kuhoji na hivyo kushindwa kutambua umuhimu na hatua mahsusi zinazochukuliwa na Serikali kurekebisha mambo yaliyofanywa na wakoloni kiuchumi na kijamii”amesema Mhe.Mwakyembe.
Dkt.Mwakyembe ameongeza kuwa wanahabri wanao wajibu wa kuilemisha jamii hasa watoto na vijana wapi Afrika imetoka ilipo na inapotaka kwenda pamoja na kulinda utamaduni wa kiafrika na kukataa kampeni za nchi za Ulaya na Marekani ambazo zinahatarisha mila na desturi zetu ikiwemo ndoa za jinsia moja pamoja na ushoga.
“Tusikubali kuingizwa huko tutamuudhi zaidi Mwenyezi Mungu,katika hili Bara la Afrika libaki kuwa safina ya Nuhu”alisisitiza Mhe.Waziri.
Vile vile Dkt. Mwakyembe amesema kuwa historia ya Ukombozi wa Bara la Afrika itasaidia wanahabari kubaini kuwa wale wanaofanya kazi ya utetetezi wa haki za
binadamu ndio waliokua watesi wa Waafrika ambao walishiriki kuasisi mifumo ya unyonyaji wa rasilimali za Afrika pamoja na ubaguzi wa rangi.