.
…………………………………………………………………..
Na Zuena Msuya, Geita
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ameviagiza vyombo vya Ulinzi na Usalama kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kumsakata na kumtia hatiani Mkandarasi Kampuni ya Cyber kwa kosa la kutapeli wananchi, kutomaliza kazi kwa wakati na kuondoka eneo husika bila taarifa yoyote.
Kampuni hiyo ya Cyber ilikuwa ikifanya kazi ya kutandaza nyaya(Wiring) katika baadhi ya nyumba za wakazi wa Kijiji cha Isabageni katika Wilaya ya Geita vijijini mkoani Geita kwa makubaliano na wananchi hao.
Dkt. Kalemani alitoa agizo hilo baada ya kusikiliza malalamiko yaliyotolewa na baadhi ya wananchi hao wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya Utekelezaji wa Mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini katika wilaya hiyo, Januari 23,2020.
Akizungumza kwa niaba ya wanakijiji wenzake, Mmoja wanakijiji hao, Samuel Mayala alimueleza Dkt. Kalemani kuwa, mkandarasi huyo alikuwa akiwatoza fedha kulingana na ukubwa wa nyumba wale wote waliokuwa wakitaka kutandaziwa nyaya katika nyumba zao kwa lengo la kuunganishiwa umeme.
Mayala aliendelea kusema kuwa, mkandarasi huyo baada ya kupokea fedha kutoka kwa wananchi alikuwa akifanya kazi hiyo bila kuikamilisha na wengine walilipia gharama hizo pasipo kufanyika kazi yeyote na baadaye mkandarasi huyo aliondoka eneo la kijiji bila taarifa zozote.
“Mheshimiwa Waziri kwa mfano mimi alinambia nilipie shilingi laki mbili na themanini, nikalipa ikabaki hamsini, akasema hawezi kumaliza kazi mpaka nimalize kulipia, nikamaliza kulipia lakini mpaka sasa sijamuona na hakumaliza kazi yangu” alisema Mayala.
Kufuatia malalamiko hayo, Dkt. Kalemani aliwaeleza TANESCO kuhakiki na kuwathibitisha wakandarasi wote wanaofanya kazi ya kutandaza nyaya katika nyumba za wanakijiji ili kuwaepusha wananchi hao na matapeli pamoja na vishoka.
Sambamba na hilo, akiwataka wananchi wote kutandaziwa nyaya katika nyumba zao na wakandarasi wanaotambuliwa na wenye uthibitisho kamili kutoka TANESCO.
Katika ziara hiyo, Dkt. Kalemani aliwasha umeme katika vijiji vitatu, vijiji viwili kati ya hivyo ni katika Wilaya ya Geita Vijijini ambavyo ni Isibageni na Bujuru, na kijiji kingine ni Mgusu wilayani Geita Mjini ambapo aliwasha umeme katika mgodi wa Aljazeera.
Meneja wa mgodi huo,Charles Nsangi aliishukuru serikali ya Awamu ya Tano, kupitia Wizara ya Nishati kwa kuwaunganishia umeme ambao utampunguza gharama za uendeshaji tofauti na ilivyokuwa hapo awali wakati akiendesha shughuli za mgodi wake kwa kutumia mafuta.
Alisema kuwa kabla ya kufungiwa umeme, alikuwa kitumia lita 40 za mafuta kila siku katika shughuli za mgodini gharama ambayo ni kubwa kulingana faida ya uzalishaji, lakini baada ya kupata umeme gharama zimepungua na kupata faida zaidi.