……………………………………………………….
Na. Edward Kondela
Serikali imesema itasimamia sheria ya ngozi nchini ya mwaka 2008 ili kuhakikisha zao hilo linaongezewa thamani kwa kuhakikisha inawatambua rasmi wachunaji wa ngozi na kuzifungia machinjio na viwanda vya ngozi visivyokuwa na wachunaji wa ngozi wanaotambulika kisheria.
Hayo yamebainishwa jana (23.01.2020) Mjini Morogoro na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega wakati wa hafla fupi ya kuzindua rasmi mafunzo ya uchunaji ngozi nchini pamoja na kukabidhi leseni kwa wahitimu 161 wa mafunzo ya uchunaji ngozi kutoka katika Manispaa ya Morogoro ambao wametakiwa kufanya kadi kwa weledi mkubwa na kutaka Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo (LITA) kuhakikisha inaendeleza elimu hiyo katika ngazi ya wilaya.
“Ninaiagiza LITA kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi ieneze katika wilaya zote mafunzo haya ili wachunaji wa ngozi wapate vitambulisho ili tusiweze kukwamisha shughuli za uchunaji wa ngozi katika wilaya zetu, mkakati wa serikali na mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli ni kuona kwamba hatuendelei kutumia fedha zetu kuagiza bidhaa za ngozi kutoka mataifa ya nje kuleta hapa Tanzania, lazima tujitosheleze sisi wenyewe na tayari ngozi zetu ziwe zimetengenezwa katika hatua ya mwisho pamoja na kutengeneza bidhaa za ngozi, tumeamua kusimama imara bidhaa za ngozi zianze kutengenezwa katika utaratibu unaotakiwa.” Amesema Mhe. Ulega
Mhe. Ulega amesema Sheria Na. 18 ya Mwaka 2008 Kifungu Na. 15 katika sheria inayosimamia biashara ya ngozi, inawataja wataalam wa uchunaji wa ngozi na kwamba kama machinjio haina wataalamu wa uchunaji ngozi au kiwanda hakina wataalam sheria inakataza.
Amefafanua kuwa sheria hiyo inaeleza wazi kuwa ikiwa mtu anafanya kazi ya kuchuna ngozi bila kutambuliwa rasmi kisheria zipo adhabu ikiwemo ya kupelekwa mahakamani ambapo kifungu kidogo cha pili kinabainisha kuwa atakayebainika kufanya kazi ya kuchuna ngozi bila kutambuliwa kisheria, atalipishwa faini ya shilingi Milioni Moja au kifungo kisichozidi Miezi Sita au adhabu zote mbili.
Naibu waziri huyo amefafanua kuwa maandalizi ya Tanzania ya viwanda ambayo ni kipaumbele cha serikali ya awamu ya tano ya kukuza viwanda nchini ambavyo vinategemea malighafi zinatokana na kilimo, mifugo na uvuvi, ngozi ni malighafi muhimu katika kutengeneza bidhaa zitokanazo na zao hilo.
“Zao la ngozi limekuwa zao muhimu katika sekta ya mifugo kwa kuliingiza pato taifa kwa mwaka 2019/20 kuanzia mwezi Julai mwaka jana hadi Desemba, Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Ngozi imepata jumla ya makusanyo ya Shilingi Bilioni 5.3, aidha zao la ngozi limeendelea kutoa ajira na kukuza kipato kwa watanzania na wafanyabiashara wa ngozi.” Amefafanua Mhe. Ulega
Awali akizungumza wakati akimkaribisha mgeni rasmi Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Mazao ya Mifugo, Usalama wa Chakula na Lishe kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Gabriel Bura amesema mafunzo yaliyotolewa ya uchunaji ngozi kwa washiriki 176 ni utekeleaji wa sheria baada ya kukutana na wadau mbalimbali ambao wamebainisha kuwa ngozi ya Tanzania ina ubora hafifu kutokana na sababu mbalimbali.
“Ngozi inaharibika kwa mfugaji kwa asilimia 30 kutokana na kupiga mfugo chapa katika maeneo yasiyofaa, mnyama kupita kwenye vichaka, lishe duni na magonjwa ya kupe na ndorobo, aidha asilimia 50 ngozi inaharibika kwenye machinjio namna mnyama anavyochinjwa na namna mchunaji anavyoichuna ngozi hiyo pamoja na vifaa anavyotumia.” Amesema Bw. Bura
Bw. Bura amesema mafunzo ya uchunaji ngozi na utoaji wa leseni tayari yametolewa katika mikoa ya Manyara, Arusha, Kilimanjaro na katika Manispaa ya Morogoro na yanatarajia kuendelea Mwezi Februari mwaka huu katika mikoa ya Kanda ya Ziwa Victoria ili wachunaji wa ngozi waweze kufanya kazi kwa mujibu kwa sheria.
Bw. Mapinduzi Ernest akizungumza kwa niaba ya wachunaji wenzake wa ngozi katika Manispaa ya Morogoro waliopatiwa mafunzo na hatimaye kukabidhiwa leseni ameishukuru serikali kwa kutoa elimu ya uchunaji bora wa ngozi ili kupandisha thamani ya ngozi ambayo inahitajika katika viwanda mbalimbali hapa nchini kutengenezea bidhaa.
Amesema ngozi ya mnyama ikichunwa vizuri itatoa tathmini ya ubora wa ngozi na kuiomba serikali kuhakikisha elimu hiyo inakuwa endelevu ili malighafi ya ngozi iweze kuwa bora zaidi.
Imetolewa: Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Mifugo na Uvuvi
24.01.2020