Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Kati, Nsolo Mlozi (wa tatu kulia) akimkabidhi mabati Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhandisi Paskas Muragili kwa ajili ya kumazia ujenzi wa vyumba vya madarasa katika wilaya hiyo. Wa pili kutoka kushoto ni Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Mkoa wa Singida, Aysharose Mattembe na kushoto ni Meneja wa Benki ya NMB Tawi la Singida, William Mponzi.
Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Kati, Nsolo Mlozi, akizungumza na Wananchi wa Kata ya Msange wakati akikabidhi msaada huo wa vifaa vya ujenzi, nondo, mabati, mbao, misumari na makowa kwa ajili ya kusaidia kumalizia ujenzi wa madarasa ya Shule ya Msingi Msange.
Wananchi wa Kata ya Msange wakiwa kwenye hafla ya kupokea msaada huo.
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Mkoa wa Singida, Aysharose Mattembe, akizungumza na Wananchi wa Kata ya Msange wakati wa hafla ya kupokea msaada huo.
Wazazi na wanafunzi wakiwa katika hafla hiyo.
Muonekano wa jengo la Zahanati ya Kijiji cha Mwachambia kilichopo Kata ya Maghojoa. Kata hiyo haina kituo cha afya wala zahanati hivyo nguvu ya pamoja inahitajika ili kumalizia jengo hilo.
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Mkoa wa Singida, Aysharose Mattembe, akiwa na wakina mama wa Kata ya Maghojoa baada ya kupokea msaada huo.
Viongozi wakiwa meza kuu wakati wa kupokea msaada huo.
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Mkoa wa Singida, Aysharose Mattembe, akisisitiza jambo kwa wananchi wa Kata ya Ngimu Kijiji cha Misuna wakati wa kupokea msaada huo.
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Mkoa wa Singida, Aysharose Mattembe, akisisitiza jambo kwa wananchi wa Kata ya Ngimu Kijiji cha Misuna wakati wa kupokea msaada huo.
Meneja wa Benki ya NMB Tawi la Singida, William Mponzi akiwaeleza wananchi wa Kata ya Msange ambao hawajafungua akaunti wakafungue katika benki hiyo.
Picha ya pamoja baada ya kupokea msaada wa vifaa vya ujenzi kwa ajili ya kumalizia Zahanati ya Kijiji cha Mwachambia. Wa pili kutoka kushoto ni Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Mkoa wa Singida, Aysharose Mattembe, wa nne kutoka kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhandisi Paskas Muragili, kulia kwa DC Muragili ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Elia Digha, Diwani wa Kata ya Maghojoa, Churi na Meneja wa Benki ya NMB Tawi la Singida, William Mponzi na viongozi wa Chama na Serikali wa wilaya hiyo.
**************************************
Na Dotto Mwaibale, Singida
BENKI ya NMB imekabidhi msaada wa vifaa vya ujenzi katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida vyenye jumla ya thamani ya shilingi milioni 20, kwa lengo la kukamilisha majengo ya zahanati na vyumba vya madarasa.
Akikabidhi msaada huo kwa Mkuu wa Wilaya hiyo, Mhandisi Paskas Muragili, Meneja wa Kanda ya Kati wa benki hiyo, Nsolo Mlozi, alisema wametoa vifaa hivyo kwa kuwa NMB ni benki inayomjali mteja na ina utaratibu wa kutenga asilimia moja ya faida inayopata na kurudisha kwa jamii
Nsolo alisema, azma ya benki hiyo mbali ya kuboresha huduma zake mbalimbali za kibenki, inajitahidi kuhakikisha ipo bega kwa bega na serikali ya Awamu ya Tano katika kuchochea na kuunga mkono juhudi za maendeleo ya kijamii na kiuchumi, hususan kwenye eneo la miundombinu ya afya na elimu.
Akipokea msaada huo, Muragili mbali ya kuishukuru NMB, aliwapongeza wananchi kwa kujitoa kama nguvu kazi kama sehemu ya kuchochea muktadha chanya wa maendeleo endelevu kwenye sekta ya elimu na afya.
“Sisi kama wilaya tupo pamoja na nyinyi, na ofisi yangu itachangia mifuko kumi ya saruji ili kusaidia kasi ya ujenzi wa matundu ya vyoo kwenye shule hii ya msingi Misuna ili kupunguza changamoto iliyopo” alisema Muragili, huku Benki hiyo ikichangia msaada wa mabati,mbao, misumari kwenye shule hiyo
Kwa upande wake, mdau mkubwa wa maendeleo, ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Singida kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Aysharose Mattembe, alisema
“kwa niaba ya wananchi wa wilaya ya Singida ninawashukuru sana benki ya NMB, kiukweli benki hii haijachangia wilaya ya Singida pekee, ikumbukwe imeshawahi pia kuchangia wilaya nyingine za mkoa wa Singida huko nyuma, ikiwemo Hospitali ya Rufaa ya mkoa wetu,” alisema na kuongeza:
“Mfano miaka minne iliyopita NMB walichangia vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni ishirini na tano katika hospitali yetu,” alisema Mattembe huku akiwataka wadau wengine wa maendeleo kuiga mfano wa benki hiyo.
Mattembe ambaye mara kwa mara amekuwa mstari wa mbele kwenye shughuli mbalimbali zenye tija mkoani hapa, aliwahimiza na kuwahamasisha wananchi ambao bado hawana akaunti NMB waende kufungua akaunti ili kuipa nguvu ya kuendelea kuchangia kwenye jamii.
Naye Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Singida, Elia Digha pamoja na kuipongeza benki hiyo, aliwataka viongozi wa NMB kusogeza zaidi huduma za kibenki kwenye maeneo ya kata na vijiji, mathalani, eneo hilo la Kata ya Msange ambalo lina wakulima wazuri wa zao la vitunguu lakini wananchi wake wanapata shida sana kupata huduma za kibenki labda mpaka wasafiri kuelekea mjini
Katika hafla hiyo ya makabidhiano shule za msingi Misuna na Msange sambamba na zahanati za Mwachambia na Mwakichenche zilikabidhiwa msaada wa mabati, nondo, misumari na mbao vyenye thamani ya shilingi milioni tano kila moja kutoka kwenye benki hiyo.