Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Arch. Elius Mwakalinga, akifafanua jambo kwa wataalamu wa Wizara ya ujenzi na taasisi zake, kuhusu uwepo wa mfumo wa kielektroniki
wa ufuatiliaji shughuli za mizani hapa nchini.
Wataalamu kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) na taasisi zake, wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Arch. Elius Mwakalinga (hayupo pichani), wakati wa kikao kazi, jijini Dodoma.
**************************
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Arch. Elius Mwakalinga, amezitaka taasisi nyingine zilizo chini ya Sekta yake kubuni na kuanzisha mifumo ya ufuatiliaji ya kieletroniki
itakayowezesha kulinda rasilimali za taasisi hizo.
Akizungumza jijini Dodoma, mara baada ya kukagua mfumo wa kielektroniki wa ufuatiliaji shughuli za mizani unaofanya kazi kwa saa 24 amezitaka taasisi hizo kuwa na ubunifu na kuwaelekeza watumishi wake kufanya kazi kwa nidhamu na uadilifu ili kuepusha vitendo vya rushwa.
“Lengo la Wizara si kukamata wafanyakazi wake na kuwachukulia hatua bali ni kujenga uwazi katika utendaji ili kuwezesha kila kinachofanyika katika taasisi hizo kufahamika kwa urahisi katika makao makuu ya
Wizara”. Amesema Arch. Mwakalinga.
Katibu Mkuu huyo amesisitiza kuwa Wizara imejipanga kufanya mabadiliko ya kiutendaji katika taasisi zake ili kuziwezesha kuingia katika uchumi wa kati kwa kuongeza mapato na tija kwa watumishi wake na Serikali kwa ujumla.
Sekta ya Ujenzi imeweka mifumo ya kieletroniki itakayosaidia kuongeza uwazi na uwajibikaji kwa watendaji wake ambapo kwa sasa vituo vya
mizani 13 vimewekewa mfumo huo wa ufuatiliaji.