Aliyepo katikati ni Msemaji Mkuu wa taasisi ya dini ya kiislamu ya Twarika ,Sheikh Haruna Hussein akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya harambee hiyo ,kushoto kwake ni Mwenyekiti wa Twarika mkoa wa Kilimanjaro,Amini Moshi huku kulia kwake akiwa ni Katibu Mkuu wa Twarika hapa nchini Khalifa Omari (Happy Lazaro)
************************************
Happy Lazaro,Arusha
Arusha.Waziri mkuu mstaafu Edward Lowasa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika harambee ya kuchangia ujenzi wa kituo cha watoto yatima itakayofanyika februari 22 mwaka huu katika Kijiji Cha Karangai wilayani Arumeru mkoani Arusha.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha ,Msemaji Mkuu wa taasisi ya dini ya kiislamu ya Twarika ,Sheikh Haruna Hussein alisema kuwa,harambee hiyo itaenda sambamba na maadhimisho ya Maulidi yatakayofanyika kijijini hapo.
Sheikh Hussein alisema kuwa,kituo hicho kwa kuanzia kinatarajia kuanza na watoto zaidi ya hamsini ambapo kitagharimu kiasi Cha shs milioni 150.
Alisema kuwa,uwepo wa kituo hicho utasaidia Sana kuondoa changamoto ya uwepo wa watoto wa mitaani ambao wamekuwa wakikosa sehemu maalumu ya kuishi na kupata huduma mbalimbali .
” tunawaomba Sana wadau mbalimbali wajitokeze katika kuchangia kituo hicho kwani huduma hiyo itatolewa kwa watu wote bila kujali dini, jambo kubwa likiwa ni kutoa huduma kwa jamii tu.”alisema Hussein.
Aidha Sheikh Hussein aliwataka viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini nchini kuungana kwa pamoja na kuombea amani Taifa linapoelekea kwenye uchaguzi Mkuu wa viongozi mbalimbali.
Sheikh Hussein alisema kuwa, ni vema viongozi wa dini wakawa wamoja na kuweka pembeni tofauti zao ili kuombea amani Taifa la Tanzania linaloelekea kwenye uchaguzi Mkuu wa Taifa.
Naye Mwenyekiti wa Twarika mkoa wa Kilimanjaro,Amini Moshi aliwataka viongozi wa dini kote nchini kuungana kwa pamoja na kuombea amani katika kipindi hiki cha Uchaguzi Mkuu wa Taifa.
Aidha aliwataka wananchi kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi katika kuchangia harambee hiyo ya watoto hao ili kuwasaidia kupata sehemu iliyo sahihi na kuweza kupata huduma zote wanazohitaji.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Twarika hapa nchini,Khalifa Omari alisema kuwa ,maadhimisho ya Maulidi ambayo ni kumbukumbu ya kuzaliwa kwa mtume Mohamedi yataadhimishwa katika Zawiya ya Karangai huku dhima ya maadhimisho hayo ni kuombea amani Taifa la Tanzania .