**********************
Na. Tamimu Adam – Jeshi la Polisi
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro kesho Januari 24, 2020 atatunuku askari Polisi Stashahada 140 na Astashahada 183 za taaluma na ujuzi wa Sayansi ya Polisi katika Mahafali ya nne ya Vyuo vya Polisi Tanzania.
Mahafali hayo ni ya nne kufanyika katika vyuo vya Polisi
Tanzania ambayo yatahusisha vyuo vinne vya polisi ambavyo ni Chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es salaam (DPA), Chuo cha Maafisa wa Polisi Kidatu (TPSC), Chuo cha Polisi Zanzibar ( ZPC) na Shule ya Polisi Tanzania ( TPS).
Katika mahafali hayo IGP Sirro atawatunuku stashahada ya upelelezi wa makosa ya jinai 101 kutoka Chuo cha maafisa wa Polisi Kidatu, stashahada ya sayansi ya polisi 39 kutoka Chuo cha taaluma ya Polisi Dar es salaam, Astashahada nyingine ni astashahada ya ujuzi wa upelelezi wa makosa ya jinai 88 kutoka Chuo cha Maafisa wa Polisi Kidatu, astashahada ya ujuzi wa Sayansi ya Polisi 18 kutoka shule ya Polisi Tanzania, Astashahada ya Mawasiliano ya Polisi 18 kutoka shule ya polisi Tanzania, na cheti cha awali cha Sayansi ya Polisi 59 kutoka shule ya Polisi Tanzania.
Mahafali hayo yatapambwa na burudani mbalimbali ikiwemo gwaride maalumu pamoja na maandamano ya wanataaluma na bodi ya ushauri ya mafunzo ya Jeshi la Polisi.