Baadhi ya washiriki wa kikao cha wadau cha kuibua maoni maalum ya kuboresha Sera ya
Maendeleo ya Wanawake na jinsia wakifuatilia kwa makini nasaha za Mgeni Rasmi wakati wa
ufunguzi wa kikao cha wadau hao katika Kanda ya Magharibi Mkoani Kigoma.
Baadhi ya wadau wa maendeleo ya jinsia kutoka Kanda ya Magharibi wakiwa katika vikundi
kazi vya kuibua maoni ya uboreshaji wa Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia katika
kikao kilichofanyika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Kigoma.
Mtaalam Mwelekezi Bi. Linah Mhando akifafanua hoja kwa wadau wa Kanda ya Magharibi
walioshiriki zoezi la kukusanya maoni kuhusu uboreshajai wa Sera ya Maendeleo ya Wanawake
na Jinsia katika ili Sera hiyo wakati wa kikao kilichofanyika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa mkoa
wa Kigoma.
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Maendeleo ya Jinsia kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto Bi. Grace Mwangwa akitao neno la utangulizi wakati wa kikao kazi
cha wadau waliokutana kutoa maoni ya kuboresha Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia
katika mikoa ya Kanda ya Magharibi mkoani kigoma.
Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma Bi. Savera Salvatory akifungua kikao kazi
cha wadau wa maendeleo ya Wanawake na Jinsia waliokutana na Wizara kujadili na kutoa
maoni ya kuhuisha Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia kwa mikoa ya Kanda ya
Magharibi mkoani Kigoma.
***************************
Na Mwandishi Wetu Kigoma
Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia ya mwaka 2000 pamoja na mapungufu ya kutekelezwa kwa muda mrefu kabla ya kuhuishwa bado imeonesha mafanikio katika kukuza ushirikishi wa wanaume, kukuza uelewa wa masuala ya wanawake na kuhimiza uzingatiaji wa
jinsia katika mipango ya kisekta.
Hayo yameelezwa na Mtaalam Mwelekezi Bi. Linah Mhando wakati akitambulisha zoezi la ukusanyaji wa maoni ya uboreshajai wa Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia ya Mwaka 2000 na Mkakati wa utekelezaji wake (2005) ili kuhuisha Sera iliyopo katika kuzingatia malengo ya mikataba ya kimataifa, Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025, Mpango wa pili wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano na mahitaji ya kijinsia.
“Sera ya Maendeleo ya Jinsia na Wanawake pamoja na mapungufu yake imeonesha mafanikio
katika eneo la ushiriki wa wanaume,imesaidia kukuza uelewa kuhusu masuala ya wanawake,
kuanzishwa kwa mifumo wezeshi, kuwa na mipango inayozingatia jinsia, kuimarisha
upatikanaji wa elimu, huduma ya miundombinu na uwezeshaji wa kiuchumi”. Alisema Bi.
Linda.
Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma Bi. Savera Salvatory amefungua kikao cha
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ambacho kinawashirikisha
wadau kutoka Kanda ya Magharibi inayojumuisha mkoa wa Rukwa, Katavi na Kigoma ambao
wamekutana kutoa maoni yao ili kuhakikisha Sera inaingiza masuala muhimu yanayochochea
kasi ya maendeleo hapa nchini na duniani kote.
Bi. Savera amewataka wadau wanaoshiriki mapitio ya sera mpya kupendekeza mikakati mipya ya kusaidia kufikia usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake.
Ameongeza kuwa kutokana na mapendekezo ya wadau Wizara imezingatia kufanya tathmini
ya kina inayozingatia masuala yote muhimu yanayopendekezwa na kuendelea kuimarisha
mengine yaliyopo ambayo yanakidhi vipaumbele vya kijinsia.
Zoezi hili linafanyika kwa kuhusisha wadau, taasisi na makundi mbalimbali katika jamii ili kuhakikisha kuwa hakuna anayeaachwa nyuma.
Mkutano wa tano unaofanyika Kanda ya Magharibi katika mkoa wa Kigoma ulitanguliwa na
Mkutano wa Kanda ya Ziwa, Kanda ya Kati, Kanda ya Kasikazini na Kanda ya Mashariki.
Mikutano hii shirikishi ilianza mwezi Septemba 2019 naitaendelea hadi Februari 2020 kwa ajili
ya kuwapa fursa wadau kutoa maoni yao katika kuzingatia usawa wa jinsia na uwezeshaji
wanawake.
Bi Severa amesema kuwa maoni yanayokusanywa kutoka kwa washiriki yatawezesha Wataalam
waelekezi pamoja na wawikilishi wa Wizara kutoa taarifa kuhusu tathmini ya jumla ya zoezi la
ukusanyaji maoni ya wadau kuhusu mafanikio na changamoto ya sera kwa kipindi cha
utekelezaji wake ili kuboresha sera iliyopo.
Mkurugenzi Msaidizi wa Maendeleo ya Jinsia Bi. Grace Mwangwa amesema kuwa Serikali inahitaji Sera ya Jinsia iliyoboreshwa ambayo inazingatia masuala jumuishi ikiwa ni pamoja na teknolojia, mabadiliko ya tabia nchi, elimu, ajira na masuala mengine ili kuingizwa kwenye
matamko ya kisera.
Wadau mbalimbali watafikiwa ili kupata wigo mpana wa ukusanyaji maoni kutoka kwa wadau wa makundi mbalimbali.
“zoezi la kuboresha sera ya maendeleo ya wanawake na jinsia ni shirikishi na tunaamini kuwa
michango ya wadau itawezesha kupata mapendekezo stahiki kwa ajili ya kuboresha sera
iliyopo”. Alisema Bi. Grace.
Bi. Grace amesema kuwa Wizara imetuma wataalam katika ngazi ya jamii ili kupata maoni yao kuhusu maeneo ya vipaumbele katika kushughulikia matatizo, changamoto zilizopo na mapendekezo ya kisera katika kuhuisha sera inayofanyiwa mapitio ili kukidhi usawa wa
kijinsia.
Naye Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka mkoa wa Rukwa Bi.Aziza Kalyatila amesema kuwa Sera
inayoandaliwa itaondoa pengo la unyanyapaa kwa wanaume na wanawake na kuwajumuisha
katika mahudhui na maelekezo ya kisera ili kwenda sambamba na juhudi za Serikali za
kupeleka maendeleo kwa makundi yote jambo ambalo litasaidia kuondokana na ukatili katika
jamii.
Kwa upande wake Meneja Biashara kutoka CRDB Bank mkoa wa Kigoma Bw. Erick Mgalla amesema kuwa wanawake wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kupata mikopo katika taasisi za kifedha maana wanawake wameachwa nyuma katika huduma za kifedha.
Amesisitiza kuwa Sera hii inapoandaliwa isaidie kuondoa vikwazo vya upatikanaji wa mikopo na huduma
ya biashara kwa wanawake ili kutoa fursa sawa kwa wanawake na wanaume.
“Kwa kiasi kikubwa wanawake wameachwa nyuma bila kupata huduma za kibiashara kutoka
taasisi za fedha. Kwa mfano masoko 254 yaliyoko katika mji wa Kigoma- Ujiji kiasi cha
asilimia 90 ya wafanyabiashara walioko katika masoko hayo ni wanawake hata hivyo kundi hili
la wanawake linachangamoto ya kukosa dhamana ya kuaminiwa na kupata mikopo na huduma
nyingine za kibiashara”. Alisema Bw. Erick.
Ameongeza kuwa Sera ya jinsia inayoboreshwa ijikite kuwanufaisha pia wanawake ili kuweza
kupata dhamana ya kumiliki ardhi na kuwezeshwa kufungua akaunti kwa kupewa haki ya
umiliki wa mali kwa mujibu wa sheria.
Mapitio ya sera yanayofanyika hivi sasa yanatoa vipaumbele katika maeneo mapya ikiwa ni
pamoja na jinsia na maendeleo ya mji/vijiji, jinsia na haki za umiliki ardhi, jinsia, maji na mazingira, haki za mtoto wa kike, jinsia na ulemavu, ukatili wa kijinsia, jinsia, sayansi ,teknolojia na ufumbuzi , jinsia, afya uzazi na ukimwi, jinsia, uongozi na maamuzi, jinsia,
ajira na kazi, jinsia, sheria na haki za binadamu na jinsia na hifadhi ya jamii.
Maeneo mengine yatakayoangaziwa ni jinsia na kuwawezesha wanawake kiuchumi, jinsia na
ujumuishwaji wa kifedha, jinsia na mabadiliko ya tabianchi, jinsia na nishati, jinsia na miundombinu, jinsia na takwimu, jinsia na madini, jinsia na vyombo vya habari na mawasiliano, jinsia na mila na desturi, jinsia na jamii za ufugaji, ufadhili na jinsia na jinsia na
uvuvi.
Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ipo katika machakato wa kukusanya maoni ya wadau kutoka katika mikoa 26 ya Tanzania Bara ili kuboresha Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia ya Mwaka 2000 kwa ajili ya kuwezesha kufikia upatikanaji wa maendeleo jumuishi kwa kuzingatia haki na usawa wa kijinsia.