Naibu Spika Dkt. Tulia Ackson amefanya ziara katika kituo kikuu cha mabasi mkoani Mbeya kwa lengo kutimiza ahadi yake ya kuwapatia jezi maalum za kuwatambulisha maafisa usafirishaji katika jiji la Mbeya maarufu kama Masalange, ili kuwaepusha na kero za kukamatwa mara kwa mara na Askari wa jiji wakiwa hawana utambulisho maalum wa kazi wanazozifanya.
Wakati huohuo Dkt. Tulia amejionea na kuelezwa changamoto mbalimbali zilizopo katika kituo hicho kikuu ikiwemo ukosefu wa maji, miundombinu mibovu ya choo, uhaba wa taa zakusaidia mwanga kipindi cha usiku, TV maalum ya kuwawezesha kufuatilia taarifa mbalimbali nchini pamoja na vitendea kazi vya kubebea mizigo ikiwemo toroli lakini Zaidi kuwezeshwa upatikanaji wa mikopo kupitia taasisi yake ya Tulia Trust.
Dkt. Tulia ameahidi kushirikiana na Maafisa hao katika kutatua changamoto hizo ambapo kwa kuanza amewakabidhi toroli moja la kubebea mizigo, kuwanunulia taa za kufunga maeneo yanayozunguka kituo hicho cha mabasi lakini pia amewaeleza kuwa atafanya jitihada za kuhakikisha huduma ya maji inapatikana kwa haraka.
“Ndugu zangu niseme tu kwamba nimezisikiliza changamoto zote na sisi kama Tulia Trust tunaahidi kushirikiana na Serikali yetu inayoongozwa na Rais John Magufuli kuhakikisha tunawakomboa vijana katika janga la umasikini, na hata hili suala la mikopo vijana wa Tulia Trust watakuja hapa na kuwapa huduma”-Dkt. Tulia