**************************
Na mwandishi wetu – Dodoma
Shilingi Bilioni 23.5 zinaokolewa kila mwaka baada ya Serikali kupitia Shirika la umeme Tanzania (TANESCO) kuzima mitambo ya kuzalisha umeme kwa kutumia mafuta mazito.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Jijini Dodoma kuhusu mafanikio ya Shirika hilo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya tano, Mkurugenzi mtendaji wa Shirika hilo Dkt. Tito Mwinuka amesema kuwa Shirika hilo limefanikiwa kujiendesha bila kupokea ruzuku kufuatia hatua zilizochukuliwa na Serikali ikiwemo kuzimwa kwa mitambo ya kuzalisha umeme kwa kutumia mafuta.
“Tumezima mitambo ya kuzalisha umeme kwa mafuta mazito katika maeneo ya Makambako, Tunduru, Liwale, Namtumbo, Ludewa, Madaba na kuyaunganisha na gridi ya Taifa hali inayochangia kuongeza kasi ya maendeleo katika maeneo hayo na kupunguza gharama za uendeshaji ;” Alisisitiza Dkt. Mwinuka
Akitaja baadhi ya mitambo iliyozimwa Dkt. Mwinuka amesema kuwa ni ile ya IPTL, AGRECO, Syimbion na mingine katika maeneo mbalimbali hapa nchini iliyokuwa ikitumia mafuta katika uzalishaji wa umeme.
Akifafanua amesema kuwa hali hiyo imechangia katika kuongeza mapato ya Shirika hilo kutoka Shilingi takribani trilioni 1.2 mwaka 2012 hadi kufikia zaidi ya trilioni 1.5 kwa mwaka kwa sasa hali inayoliwezesha Shirika hilo kuendelea kuongeza tija katika utoaji wa huduma.
Kwa upande wa wateja waliounganishiwa umeme wameongezeka kutoka milioni 1.6 waliokuwepo kufikia mwaka 2015 hadi zaidi ya milioni 2.7 kufikia mwaka 2019 sawa na ongezeko la wateja zaidi ya milioni 1.05 katika kipindi hicho ambao ni asilimia 63.84.
Akizungumzia miradi ya kimkakati Dkt. Mwinuka amesema kuwa ni pamoja na mradi wa kufua umeme wa Mwalimu Nyerere katika Mto Rufiji megawati 2115 unaotekelezwa na Serikali kwa gharama ya shilingi trilioni 6.55, Rusumo megawati 80, Kakono megawati 87, Mradi wa kuzalisha umeme kwa gesi mkoani Mtwara megawati 300.
Akieleza zaidi, Dkt. Mwinuka amesema kuwa miradi mingine inatekelezwa katika maeneo mengine katika mikoa mbalimbali hapa nchini kwa lengo la kuhakikisha kuwa kila mwananchi anafikiwa na huduma ya umeme.
Kwa upande wa Vijiji vilivyounganishiwa umeme vimeongezeka kutoka 2018 mwaka 2015 hadi Vijiji 8236 kufikia Desemba 2019 ikiwa ni ongezeko la asimia 67 hali inayotokana na jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano kuhakikisha kuwa wananchi wote wanafikiwa na nishati ya umeme katika maeneo yote.
Katika kipindi cha miaka 4 umeme ulioongezwa kwenye gridi ya Taifa ni Megawati 400 zinazotokana na utekelezaji wa miradi ya kimkakati ikiwemo ya Kinyerezi namba 1 na namba 2.
“Kwa upande wa wateja wa viwanda wameongezeka kutoka 2571 mwaka 2015 hadi 3787 mwezi Desemba 2019;” Alisisitiza Dkt. Mwinuka
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limetekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ya uzalishaji, usambazaji na uwekezaji katika sekta ya nishati ili kukuza uchumi na ustawi wa wananchi.