Mwalimu Mkuu wa shule ya sekondari ya Oldonyowas iliyopo wilayani Arumeru mkoani Arusha akizungumza na wanafunzi wa shule hiyo Jana .(Happy Lazaro).
***********************************
Happy Lazaro, Arusha
Arusha.Uongozi wa kata ya Oldonyowas katika Halmashauri ya Arusha wanaanza msako rasmi wiki hii kwa ajili ya kubaini watoto 80 ambao hawajaripoti katika shule ya sekondari Oldonyowas walipopangiwa kuingia kidato cha kwanza mwaka huu.
Akizungumza leo na waandishi wa habari shuleni hapo,Mkuu wa shule hiyo Richard Mugyabuso amesema kuwa,katika matokeo ya darasa la Saba mwaka Jana jumla ya watoto 169 walipangiwa kujiunga na shule hiyo lakini hadi Sasa hivi ni watoto 89 tu ambao wameripoti.
Mugyabuso amesema kuwa,nusu ya wanafunzi hao waliopangiwa hawajaripoti shuleni mpaka Sasa hivi na hawajulikani walipo na hata taarifa zao hakuna.
Amesema kuwa,kutokana na swala hilo kuanzia wiki hii uongozi wa kijiji hicho wataanza msako wa nyumba kwa nyumba kwa ajili ya kuwakagua wanafunzi hao walipo na mzazi atakayekutwa na mtoto bila sababu za msingi atachukuliwa hatua za kisheria.
“yaani wiki nzima hii tunapita kila nyumba tunaomba kama Kuna mzazi ambaye mtoto wake yupo nyumbani na hadi sasa hivi hajaripoti shuleni afanye hivyo kabla ya jumatatu kwani hatutakuwa na huruma na mzazi yeyote ambaye hataki mtoto aende shuleni kwa sababu zake binafsi.’amesema Mugyabuso.
Naye Afisa elimu kata ya Oldonyowas ,Jacob Jackson amesema kuwa,ni muda wa wiki mbili Sasa tangu shule zimefunguliwa lakini wanashangazwa na baadhi ya wazazi kutowaruhusu watoto wao kuripoti shuleni bila sababu zozote.
Jacob amesema kuwa,wiki hii viongozi wa kata hiyo wakishirikiana na Mtendaji wa kata watafanya msako wa nyumba kwa nyumba kutafuta wanafunzi hao kwani kwa kata nzima wanafunzi waliopangiwa shuleni hapo ni 169.
“kila mmoja anatambua serikali ya awamu ya tano haitaki mchezo na swala la elimu ,Sasa ni juhudi za serikali ngazi ya kata kuhakikisha Kila mwanafunzi anaripoti shuleni kwani hakuna Cha kujitetea elimu ni bure”amesema Jacob.
Mwenyekiti wa kijiji Cha Oldonyowas ,Jofrey Ayo amesema kuwa,kumekuwepo na changamoto kubwa Sana ya mwamko mdogo wa elimu kwa jamii hiyo ya wafugaji kwani wengi wao hushindwa kuwapeleka shule kutokana na mila na desturi ikiwemo kuwaozesha wakiwa wadogo.
“Sasa tunafanya msako ole wa mzazi ambaye tutamkuta na mtoto nyumbani kwani wanafunzi walishaanza masomo wiki ya pili Sasa hivyo wenzao wameshawapita Sana,Kama Kuna mzazi ambaye hajamleta shuleni mtoto wake wahakikishe wanawaruhusu haraka sana kabla ya jumatatu.’amesema Ayo.