Kazi ya uchimbaji wa msingi kwa ajili ya kusimika nguzo za chuma katika Mradi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Bulyanhulu hadi Geita ikiendelea. Taswira hii ilichukuliwa Januari 20, mwaka huu wakati Kamishna Msaidizi wa Umeme, Mhandisi Innocent Luoga alipotembelea Mradi huo.
Kamishna Msaidizi wa Umeme, Mhandisi Innocent Luoga (katikati), akitoa maagizo kwa Mkandarasi anayetekeleza Mradi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Bulyanhulu hadi Geita.
Hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Bulyanhulu.
**********************************
Na Mwandishi Wetu
Kamishna Msaidizi wa Umeme Mhandisi Innocent Luoga, amefanya ziara ya kukagua utekelezaji wa Mradi wa ujenzi wa Njia ya Kusafirisha Umeme ya msongo wa kilovoti 220 inayoanzia Bulyanhulu hadi Geita na kumtaka Mkandarasi kuanza kazi ya kusimika nguzo za chuma ifikapo Februari 2020.
Mhandisi Luoga alifanya ziara hiyo Januari 20, 2020 kukagua Mradi huo ambao unahusisha pia ujenzi wa vituo vya kupoza Umeme katika eneo la Bulyanhulu, Wilayani Kahama na katika Mkoa wa Geita, pamoja na kusambaza umeme katika vijiji 10 vinavyopitiwa na Mradi huo.
“Nimeridhishwa na kasi ya ujenzi wa vituo vya kupoza umeme vya Bulyanhulu na Geita lakini sijaridhishwa na kazi ya usimikaji wa nguzo za kusafirisha Umeme ambapo misingi 52 kati ya misingi 161 imekamilika na hakuna nguzo iliyosimamishwa. Nawataka Mkandarasi na Mhandisi Mshauri kujipanga upya ili Mradi huo wenye lengo la kuimarisha upatikanaji wa umeme katika Wilaya za Kahama, Geita, Chato, Biharamulo na Ngara pamoja na kuunganisha Mkoa wa Geita katika Gridi ya Taifa ukamilike kwa wakati.”
Aidha, Mhandisi Luoga alimuagiza Mkandarasi kufanya kazi siku zote, kuongeza idadi ya mafundi na vifaa maalum vya kuchimba katika miamba ili kuhakikisha nguzo zinaanza kusimamishwa ifikapo Februari 2020 na Mradi huo unakuwa tayari kusafirisha umeme .
Akitoa maelezo kwa Kamishna, Mhandisi wa Mradi Ramadhani Kidunda alisema Mradi huo unatarajiwa kukamilika tarehe 30 Mei 2020 na utahusisha pia kusambaza Umeme katika vijiji 10 vinavyopitiwa na Mradi husika pamoja na Vituo vya kupoza Umeme katika eneo la Bulyanhulu na GEITA .
Kamishna Luoga aliwataka Mameneja wa TANESCO wa Mikoa ya Shinyanga na Geita kuhakikisha wanafanya usanifu wa kutosha ili migodi iliyopo katika Mikoa ya Geita na Shinyanga ikiwemo Geita Gold Mining (GGM), Bulyanhulu na STAMIGOLD inapatiwa umeme wa uhakika pamoja na vijiji vyote vinavyopitiwa na Mradi huo ambavyo havina Umeme na kuvipatia umeme kupitia Mradi huo bila kuruka kijiji chochote.
Aidha, aliitaka TANESCO kumsimamia Mkandarasi kikamilifu ili kuhakikisha Mradi unatekelezwa katika ubora na viwango vinavyotakiwa.
Katika ziara hiyo, Kamishna Msaidizi wa Umeme Mhandisi Innocent Luoga, aliambatana na Mhandisi wa Mradi huo, Mhandisi Ramadhani Kidunda, Meneja wa TANESCO wa Mkoa wa Shinyanga, Meneja wa Wilaya ya Kahama pamoja na Mkandarasi anayetekeleza Mradi huo ambaye ni M/s CAMC Engineering Co Ltd ya China na Mhandisi Mshauri M/s SHAKER ya Misri.