**********************************
NA MWAMVUA MWINYI,PWANI
MWANAFUNZI wa darasa la pili katika shule ya msingi Jitegemee,huko Mwendapole Kibaha mkoani Pwani,amekutwa ameuawa na mwili wake kutupwa katika nyumba ambayo haijakamilika ujenzi, mauaji yanayodaiwa kutokea baada ya kubakwa kutokana na kukutwa na michubuko sehemu zake za siri .
Mtoto huyo anadaiwa kuuawa siku chache zilizopita na jina lake limehifadhiwa.
Kamanda wa polisi mkoani Pwani,Wankyo Nyigesa amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema jeshi la polisi mkoani hapo linaendelea kuwasaka watuhumiwa waliohusika na uhalifu huo wa kikatili .
Wankyo alifafanua,awali kabla ya mauaji January 14 asubuhi, marehemu aliondoka na shangazi yake Agnes Fusi kuelekea gulioni eneo la Mwendapole kwa shughuli za biashara ndogondogo.
“Mtoto huyo (jina tunalihifadhi)aliruhusiwa kurejea na shangazi yake majira ya saa 18:30 kwa ajili ya maandalizi ya shughuli za kesho “Baada ya shughuli za biashara shangazi yake na marehemu alirejea nyumbani na hakumkuta mtoto.”
Jitihada za kumtafuta ziliendelea maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa jeshi la polisi.
Kamanda huyo wa polisi ,Wankyo alieleza ilipofika January 19 majira ya saa moja mtoto huyo aliokotwa katika nyumba inayoendelea kujengwa (pagale)akiwa ameuawa huku akiwa na michubuko sehemu za siri kuashiria kwamba alibakwa kabla ya kuuawa.
Wankyo aliwataka wenye taarifa yoyote ya tukio hilo kutoa taarifa kwa jeshi hilo,vyombo vingine vya dola na kwa serikali za mitaa.
Aliwaomba wazazi na walezi kwenye jamii wasiwache na kuwaamini watoto wenye umri mdogo peke yao bila uangalizi wala usimamizo wa karibu.
Alikemea wanaume pia wenye roho za kikatili kama hizo endapo kweli yupo aliyefanya tukio hilo na kueleza ni tukio la kinyama.
Nae mkazi wa Mwendapole mama Kadibo alisema ,mtoto huyo amezikwa leo,huku tukio hilo likisikitisha jamii inayomzunguka kutokana na kifo chake.