************************************
Na Mwandishi Wetu, Pemba
WATU wanaodaiwa kuwa wafuasi wa Chama cha ACT-
Wazalendo, usiku wa kuamkia jana wamechoma moto nyumba ya Katibu wa Jumuia ya Wazazi wa Chma Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya Micheweni Mkoa Kaskazini Pemba, Nassor Seif Said.
Tukio hilo limetokea saa chache baada ya kuripotiwa zoezi la uandikishaji wapiga kura katika Daftari la Wapiga Kura kwenda vizuri kwenye baadhi ya maeneo katika Wilaya ya Micheweni kisiwani hapa.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, walisema
waliochoma moto nyumba ya Sheha walifanya hivyo baada ya kushindwa kupandikiza watu kwenye zoezi la uandikishaji katika Shehia ya Wingwi Mapofu.
Kamanda wa Polisi Mkoa Kaskazini Pemba, Juma Sadi, alisema hadi sasa wamewakamata watu watano kwa tuhuma za kuhusika na tukio hilo na upelelezi zaidi unaendelea.
Kamanda Sadi alisema tukio hilo limetokea saa 2 usiku, katika Kijiji cha Simai, Shehia ya Wingwi Mapofu, Wilaya ya Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba.
“Watu hao wa mihemko ya kisiasa walichoma moto nyumba ya Katibu wa Jumuia ya Wazazi CCM, Nassor Seif Said.
“Tukio hili limefanywa kwa misingi ya kisiasa, tunaendelea na uchunguzi, kuna watuhumiwa watano tunawashikilia, upelelezi ukikamilika tutawafikisha Mahakamani,” alisema.
Alisema tayari jeshi hilo linawashikilia viongozi wa chama hicho Wilaya ya Micheweni kwa tuhuma za kuhusika na tukio hilo. Viongozi hao ni Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Mkoa wa Kaskazini Pemba, Rashid Khalid Salim, Katibu wa Mipango na Uchaguzi wa chama hicho Kaskazini Pemba, Abdallah Ali Said.
Wengine ni Katibu wa Wadi ya Mapofu wa chama hicho Jimbo la Wingwi, Ali Rajab Kombo, Katibu wa Mipango na Chaguzi wa chama hicho Jimbo la Wingwi, Haban Salum Sleyum, mfuasi wa ACT Jimbo la Wingwi, Said Faki Dadi na Ali Saleh Juma mkazi wa Wingwi.
Aliongeza kuwa, hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote ambaye atabainika kuhusika na tukio hilo, kuwaonya wananchi waache mara moja vitendo vya uvunjifu wa amani.
Alisema jeshi lake limejipanga kupambana na yoyote ambaye atajaribu kuhatarisha amani ya nchi.
Akizungumzia tukio la nyumba yake kuchomwa moto, Said
alisema limechangiwa na choko choko ya wanasiasa na kuiomba Serikali kuwachukulia hatua kali viongozi wa ACT-Wazalendo waliohamasisha fujo na uvunjifu wa amani katika nchi.
“Waliofanya hivi ni watu wa upinzani kutoka ACT-Wazalendo, maana wanaona mimi kikwazo katika kufanikisha mipango yao ya kutaka waandikishwe watu kutoka Tanga na wasio na sifa ya kuandikishwa katika daftari,” alisema Said.
Alifafanua kuwa, licha ya vitisho na kuchomewa moto nyumba yake kamwe hatorudi nyuma, atasimama katika misingi ya sheria kuhakikisha asiye ya sifa haandikishwi.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa CCM, Wilaya ya
Micheweni, Maryam Omar Ali, ameviomba vyombo vya ulinzi na usalama Kisiwani Pemba kuhakikisha wako macho katika kipindi chote cha uandikishaji kwani kuna dalili za kufanyika hujuma zinazopangwa na wanachama wa ACT-Wazalendo.
“Tumeviomba vyombo vyetu vya ulinzi na kuwaambia wasione utulivu uliokuwapo jana ukawapa matumaini, hatujui wenzetu wamejipanga vipi,” alisisitiza Ali.