Home Mchanganyiko WAZIRI UMMY AZINDUA KAMPENI YA KIPEPEO MKOANI MOROGORO

WAZIRI UMMY AZINDUA KAMPENI YA KIPEPEO MKOANI MOROGORO

0

Mhe. Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu leo hii amezindua Kampeni ya Kipepeo Mkoani Morogoro. Kampeni hii inatekelezwa kwa ushirikiano wa Wizara ya Afya, Jinsia, Wazee na Watoto kupitia Mpango wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI (NACP) na Taasisi ya Benjamin William Mkapa.

Mhe. Ummy Mwalimu amesema lengo la Kampeni hii ni kuwasaidia wanafunzi hasa wa kike kujitambua, kujiamini na kuongeza bidii ya kujenga ndoto zao sambamba na kuwapatia mbinu za namna ya kupambana na changamoto mbalimbali za kimaisha, kimasomo na vishawishi vinavyoweza kuwapotezea muelekeo na kushindwa kufikia ndoto zao.

Waziri ameongeza kuwa Wizara yake ikishirikiana na taasisi na wadau wa Afya ina lenga kuifanya Kipepeo kuwa kubwa zaidi ili kuwafikia wanafunzi wengi zaidi wa rika balehe wanaosoma shule za sekondari kwa ajili ya kuwafikishia elimu kuhusu maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU), athari za mimba za utotoni, matumizi sahihi ya ARV kwa wale walioathirika tayari sambamba na kueneza elimu dhidi ya unyanyapaa.


Nae Mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Benjamin William Mkapa amesema Kampeni ya Kipepeo itafanyika kwenye jumla ya mikoa kumi (10) ambapo vigezo vya kuchagua Mikoa husika ni viwili; kwanza ni kwa kuzingatia mikoa yenye kiwango cha juu cha maambukizi ya VVU kwa kundi linalolengwa. Pili, mikoa yenye kiwango cha juu cha mimba za utotoni. Mikoa hiyo ni pamoja na Mbeya, Iringa, Njombe, Mwanza, Dodoma, Tanga, Arusha, Mtwara, Morogoro na Singida.


Mkuu wa Mkoa wa Morogoro amesema Mkoa wake unaunga mkono hii Kampeni kwakuwa kupitia kampeni kama hizi Mkoa umefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutoa elimu kwa wananchi juu ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU), athari za mimba za utotoni, matumizi sahihi ya ARV kwa wale walioathirika tayari sambamba na kueneza elimu dhidi ya unyanyapaa.