*********************************
Na.Catherine Sungura,Dodoma
Viongozi wa vikundi kazi vya kitaaluma nchini wametakiwa,kuhakikisha malengo ya mipango mkakati wa sekta ya afya yanatekelezwa ipasavyo.
Rai hiyo imetolewa jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Zainab Chaula wakati wa kikao cha mashirikiano baina ya serikali na wadau wa sekta ya afya nchini Tanzania (Health SWAP in Tanzania) kilichofanyika jijini hapa.
Dkt. Chaula amesema kuwa viongozi wote wanatakiwa kutekeleza wajibu wao kulingana na taratibu ambazo wamejiwekea kwa kuhakikisha wao kama viongozi wa vikundi kazi toka serikalini wanakuwa mstari wa mbele katika kutoa dira na mwelekeo wa utekelezaji wa malengo yote ya kimkakati katika sekta ya afya.
“Nina imani mtaendelea kuboresha utendaji kazi wa vikundi kazi hivi kwa kushirikiana na wadau wengine pamoja na kutoa ushauri wa kitaalam katika maeneo ya kimkakati ya uboreshaji wa huduma”.Alisisitiza Dkt. Chaula
Aidha, Katibu mkuu huyo aliwataka viongozi hao kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kuandaa mpango mkakati wa sekta ya afya wa awamu ya tano(2020-2025) na kutoa maoni na mapendekezo ya idadi ya vikundi kazi zilizowasilishwa na.idara ya sera na mipango wizarani hapo.
Serikali ya Tanzania ilianza utekekezaji wa mashirikiano katika sekta ya afya na wadau mbalimbali wakiwemo wadau wa maendeleo,mashirika yasiyo ya kiserikali,asasi za kiraia na wizara mbazo zinatekeleza shughuli za sekta ya afya mwaka 1999.