Na Mwandishi wetu Mihambwe
Afisa Tarafa Mihambwe, Emmanuel Shilatu leo amefanya ziara kutembelea maeneo mbalimbali ya Tarafa ya Mihambwe kwenye vituo vya uandikishaji kwenye daftari la kudumu la wapiga kura na kuridhishwa na zoezi linavyoendelea kwa hali ya amani na utulivu.
Gavana Shilatu amefika kwenye maeneo hayo ili kujionea zoezi linavyoendeshwa na kuwauliza Wananchi aliowakuta juu ya utolewaji wa huduma kama wanapata changamoto yeyote ile na kukiri zoezi linaenda vyema kwa amani pasipo changamoto yeyote ile.
Zoezi hilo la uboreshaji taarifa kwenye daftari la kudumu la wapiga kura limeanza Januari 12, 2020 na litaisha Januari 18, 2020 na kuwasihi Wananchi kuhimizana kujitokeza kwa wingi kuboresha taarifa zao.
Akizungumza mara baada ya ukaguzi huo Gavana Shilatu amekiri kuridhishwa na namna zoezi linavyoendeshwa kwa hali ya utulivu na kuwasihi Wananchi kutoa ushirikiano wa kutosha kwenye zoezi hili.
“Maeneo mbalimbali ndani ya Tarafa ya Mihambwe zoezi linaenda vyema kwa utulivu mkubwa. Nitoe rai Wananchi wenye umri wa miaka 18 na kuendelea kujitokeza kujiandikisha ama kuboresha taarifa zao kwenye daftari la kudumu la Wapiga kura ili kupata fursa ya kumchagua Diwani, Mbunge na Rais kwenye uchaguzi mkuu mwaka huu 2020.” Alisema Gavana Shilatu.
Nae Mwananchi aliyejitokeza kuboresha taarifa zake ameridhishwa na zoezi linavyoendelea kwa amani na utulivu.
“Kikubwa hapa ni zoezi kuendeshwa kwa utulivu na utaratibu mzuri huku tukimuona Afisa Tarafa akipita mara kwa mara kuona zoezi linaenda vyema, tunaridhishwa na utendaji wake. Tuna kila sababu Watanzania kujivunia amani na utulivu tulionao unaotuwezesha kufanya mambo yetu kwa raha tupu na Uhuru.” Alisisitiza Mzee Kadogo Nantave mmoja wa Wananchi waliojitokeza kuboresha taarifa yake.