Home Mchanganyiko DKT. KIJAZI AWATAKA WATENDAJI WA SHIRIKA LA HALI YA HEWA DUNIANI (WMO)...

DKT. KIJAZI AWATAKA WATENDAJI WA SHIRIKA LA HALI YA HEWA DUNIANI (WMO) KUANDAA MPANGO WA PAMOJA WA KUBORESHA ZAIDI UAANDAAJI NA UWASILISHWAJI WA TAARIFA ZA HALI YA HEWA KWA JAMII ZILIZO KATIKA MAZINGIRA HATARISHI

0

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirikia la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Agnes Lawrence Kijazi akichangia mada wakati wa mkutano. Kushoto kwake (aliyevaa miwani) ni Makamu wa Pili wa Rais wa WMO, Ndugu Albert Martis.

Viongozi Wandamizi wa Shirikia la Hali ya Hewa Duniani (WMO) wakifuatlia mjadala wakati wa mkutano. Meza ya mbele, kutoka upande wa kulia ni Katibu Mkuu wa WMO, Prof. Petteri Taalas, anayemfuatia(aliyevaa tai nyeusi) ni Rais wa WMO Prof. Gerhard Adrian. Meza ya pili kutoka upande wa kulia, wa kwanza ni Makamu wa 3 wa Rais wa WMO, Prof. Celeste Saulo; anayemfuatia  ni Makamu wa Pili wa Rais wa WMO, Ndugu Albert Martis, na anayefuata ni Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirikia la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Agnes Lawrence Kijazi.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirikia la Hali ya Hewa Duniani (WMO) akifafanua jambo walipokutana na Mkurugenzi wa Taasisi ya Hali ya Hewa ya Canada (ambaye pia ni msaidizi wa Naibu Waziri mwenye dhamana ya masuala ya hali ya hewa), Bi. Diane Campbell kwa maongezi mafupi wakati wa mapumziko nje ya ukumbi wa mkutano. Bi Diane, alitaka kufahamu tafasili ya mabadiliko ya kimuundo yaliyofanywa na WMO na majukumu ya nchi wanachama katika utekelezaji wa mabadiliko hayo.

*********************************

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirikia la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Agnes Lawrence Kijazi, amewataka watendaji wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) kuandaa mpango wa kuboresha zaidi uaandaaji na uwasilishwaji  wa taarifa za hali ya hewa kwa jamii zinazoishi katika mazingira hatarishi ya kukumbwa na majanga yanayotokana  na hali mbaya ya hewa, utakaotekelezwa kwa pamoja ili kuziwezesha jamii hizo kupunguza vihatarishi vya kukumbwa na maafa. Dkt. Kijazi ameyasema hayo wakati akichangia mada katika mkutano ulioandaliwa na WMO kwa kushirikiana na Taasisi ya Hali ya hewa ya Marekani “National Oceanic and Atmospheric Administration (NOAA)- National Weather Service”, uliofanyika tarehe 11 Januari, 2020 Boston, nchini Marekani. 

Lengo la mkutano huo  lilikuwa kujadili uboreshaji wa uandaaji na uwasilishwaji wa taarifa za hali ya hewa  kwa jamii zinazoishi katika mazingira hatarishi, hususan visiwa vilivyopo katika ukanda wa tropic na arctic (Improving Communication and Preparedness in Vulnerable Regions and Underserved Communities of the tropical and Arctic region islands), ambavyo viko katika mazingira hatarishi ya kukumbwa na vimbunga na mawimbi ya tsunami. Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi waandamizi wa WMO, ikiwa ni pamoja na Rais wa WMO (Prof. Gerhard Adrian), Makamu wa kwanza wa Rais wa WMO (Prof. Celeste Saulo), Makamu wa Pili wa Rais wa WMO (Ndugu Albert Martis), Makamu wa Tatu wa Rais wa WMO (Dkt. Agnes Kijazi) na Katibu Mkuu wa WMO, Prof. Petteri Taalas; Wakuu wa Taasisi za hali ya hewa kutoka baadhi ya nchi wanachama wa WMO; na wadau wa huduma za hali ya hewa, miongoni mwao sekta binafisi na watafiti kutoka vyuo vikuu.  

Majadiliano ya mkutano huo yalijielekeza zaidi katika matokeo ya tafiti zilizofanyika katika nchi za Guyana, Finland, Indonesia, Marekani (Jimbo la Alaska), visiwa vya Caribbean na Bahamas, pamoja na eneo la Pacific zilizowasilishwa. Tafiti hizo ziliainisha changamoto katika uandaaji na uwasilishwaji wa taarifa za hali ya hewa kwa jamii zinazoishi katika mazingira hatalishi ya kukumbwa na majanga yanayotokana na hali mbaya ya hewa, ambayo hutokea katika maeneo hayo. Aidha, tafiti hizo ziliainisha njia za asili zinazotumiwa na jamii hizo katika kuchukua tahadhari  na kutoa mapendekezo ya kuboresha ili kupunguza maafa yanayotokana na majanga hayo.  

Akichangia mada, Dkt. Kijazi alifafanua kwamba kwa kuwa changamoto zilizowasilishwa zinaweza kuwepo katika maeneo mengi, yakiwemo maeneo yanayofanana na hayo yaliyopo katika bara la Afrika, ni vyema kuandaa mpango wa pamoja utakaoratibiwa na WMO wa kushughulikia changamoto hizo. Hivyo, akawataka watendaji wa WMO kuangalia uwezekano wa kuandaa mpango huo ili kuboresha zaidi uaandaaji na uwasilishwaji  wa taarifa za hali ya hewa kwa jamii husika. Ili kuharakisha utatuzi wa changamoto  zilizowasilishwa, viongozi waandamizi wa WMO (Rais, Makamu wa Rais wote watatu na Katibu Mkuu) wameazimia kufanya vikao kwa njia ya mtandao (teleconference) kila mwisho wa mwezi, kuanzia mwezi Januari 2020.

Mkutano huu ni sehemu ya mkutano mkuu wa 100 wa wadau wa huduma za hali ya hewa wa Marekani  unaofanyika Boston, Marekani kuanzia tarehe 10 hadi 16 Januari, 2020 kujadili utekelezaji wa maazimio ya mkutano mkuu wa WMO uliofanyika Juni 2019. Dkt. Kijazi anashiriki katika mkutano huo kama Makamu wa Tatu wa Rais wa WMO.