Baadhi ya Maofisa habari na wanahabari wakifuatilia Naibu Mkurugenzi wa Hospitali hiyo(hayupo pichani) wakati akitoa taarifa ya maboresho yaliyofanywa katika hospitali ya Muhimbili Mloganzila
Muuguzi Rose Chasuka akielezea namna mashine ya kupima mapafu inavyofanya kazi wakati wa ziara hiyo
Mtaalam kutoka kitengo cha Radiolojia MNH-Mloganzila, Dkt. Ahmed Sauko akielezea namna mashine ya MRI inavyofanya kazi
Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila, Dkt. Julieth Magandi (katikati) akitoa taarifa wakati wa ziara hiyo
Mmoja wa wanahabari akiwa kwenye mashine ya kupima mapafu akionesha namna ya mashine hiyo inavyofanya kazi wakati wa ziara hiyo. Mashine hiyo ni miongoni mwa mashine pekee hapa nchini.
*****************************
HOSPITALI ya Rufaa ya Taaluma na Tiba ya Mloganzila (MAMC) inatarajia kujenga kituo cha Umahiri cha upandikizaji Viungo (Centre of Excellence for Organ Transplant ) kitakachosaidia kupunguza gharama kwa Watanzania walizokuwa wakizifuata nje ya Nchi.
Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili- Mloganzila, Dkt.Julieth Magandi amesema hayo leo wakati wa ziara ya Maafisa habari wa Wizara ya afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Taasisi zake katika muendelezo wa kampeni ya kutangaza mafanikio ya Serikali ya awamu ya Tano inayojulikana kama ‘TUNABORESHA SEKTA YA AFYA’.
Dkt. Magandi amebainisha kuwa, tayari bajeti ya fedha imetengwa na Serikali ya Awamu ya Tano na kinatarajiwa kujengwa katika eneo jirani na Hospitali hiyo ya Mloganzila.
“Katika mwaka wa fedha 2019/2020 Serikali imetenga fedha kiasi cha Tsh. Bilioni 8 kwa ajili ya uanzishwaji wa kituo cha Umahiri cha Upandikizaji viungo.
Kitaalamu tunaita ‘Centre Excellence for Organ Transplant’ na vitu vingi vitapandikizwa hapa” alisema Dkt. Magandi.
Amevitaja viungo ambavyo vitapandikizwa katika kituo hicho kitakapokamilika ni pamoja na Upandikizaji wa Ujauzito (In Vitro fertilization-IVF) kupandikiza Uloto (Bone marrow), upandikizaji wa Ini (Liver Transplant), Macho (Corneal transplant), Figo (Kideney transplant).
pamoja na kituo cha wataalam kujifunzia (Skills lab).
Aidha, akielezea mipango iliyopo ya hospitali hiyo ni pamoja na ujio wa huduma ya upandikizaji Uloto (Bone marrow transplant) huduma ambayo itaanza kutolewa kwa mara ya kwanza hapa nchini.
“Katika maboresho na kuongeza huduma kwa Watanzania. Muhimbili-Mloganzila kwa kushirikiana na Muhimbili-Upanga tunatarajia kuanzisha huduma ya upandikizaji Uloto. Huduma hii itaanza kutolewa Februari mwaka huu na hii itakuwa ya kwanza hapa nchini kwani haikuwepo hapa nchini”. Alisema Dkt. Magandi.
Hata hivyo katika kuboresha huduma za Wagonjwa mahututi (ICU), wapo mbioni kupokea wataalam Sita kutoka Nchi ya Cuba ambao wamebobea kwenye huduma hizo huku pia wakitarajia kuwa msaada mkubwa kwa wataalam wazawa wa ndani ambao watapata ujuzi kutoka kwao.
Hadi sasa Hospitali hiyo imekuwa ikipokea wagonjwa mbalimbali wanaohudumiwa kwenye kitengo hicho.
Hospitali hiyo ya Muhimbili-Mloganzila ilifunguliwa rasmi Novemba 2017 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ikiwa chini ya uendeshaji wa Chuo kikuu cha Afya na tiba shirikishi cha Muhimbili (MUHAS) iliyo chini ya wizara ya Elimu, sayansi na teknolojia na baadae Oktoba 3,2018 ilikuja kubadilishwa usimamizi na uendeshaji na kuhamishiwa wizara ya Afya na kuwa chini ya Hospitali ya Taifa Muhimbili hivyo kuitwa ‘Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila.