Mbunge wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu amekabidhi mifuko 100 ya saruji yenye thamani ya shilingi milioni 1.6 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa nyumba ya Mapadri katika kanisa Katoliki Parokia ya Kibaoni mkoani Singida ikiwa ni utekelezaji wa ahadi yake aliyoitoa mwaka jana.
Akikabidhi msaada huo Mtaturu amemshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumuwezesha kutimiza ahadi yake.
“Mwaka jana nilitoa ahadi hii na leo nafurahi na kumshukuru Mungu kwa kuniwezesha kutimiza kile nilichoahidi,”alisema Mtaturu.
Amewaasa watanzania kuendelea kuishi kwa upendo na kuimarisha amani ya nchi na kuendelea kumuombea Rais dkt John Magufuli afya njema ili aendelee kuiongoza nchi kwenye maendeleo.
“Rais wetu dkt John Magufuli anafanya kazi nzuri kwa niaba ya watanzania,hivyo tusiruhusu watu wasio na nia njema na nchi yetu kutugawa,”alisisitiza mbunge huyo.
Ili kuunga mkono hatua hiyo waumini wa kanisa hilo walichangia shilingi milioni 2.1 na kumshukuru mbunge huyo kwa moyo wake wa majitoleo.
Kwa upande wake Paroko wa Parokia ya Kibaoni Patrick Nkokho akizungumza kwa niaba ya Parokia amemshukuru mbunge huyo kwa uamuzi wake wa kuchangia saruji ili kukamilisha ujenzu huo.