Home Mchanganyiko APATIWA DHAMANA KWA MAHAKAMA MTANDAO

APATIWA DHAMANA KWA MAHAKAMA MTANDAO

0

Maafisa wa magereza wakifuatilia mashauri kwa njia Mahakama Mtandao (kushoto) Musa Kaswaka na (kulia) kwake ni George Mwambashi yaliyokuwa yakiendeshwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya wananchi waliofika katika ukumbi wa mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, iliyopo jijini Dar es Salaam wakifuatilia mwenendo wa uendeshaji mashauri kwa njia ya Mahakama Mtandao.

Picha ya pamoja ikionyesha washiriki wa zoezi la mahakama mtandao katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na Gereza la Keko jijini Dar es Salaam.

**************************************

Na Innocent Kansha na Salum Tawani

Mahakama ya Hakimu .Mkazi Kisutu iliyopo Jijini Dar es Salaam leo  kwa mara ya kwanza imetoa  dhamana ya mahabusu Bw. Abubakari  Seguni aliyepo katika  Gereza la Keko kwa njia ya Mahakama Mtandao maarufu kama ‘Video Conference’.

Dhamana hiyo imetolewa na Mahakama hiyo kwa kushirikiana na Gereza la Keko lilipo katika jiji hilo, wakati ilipokuwa  ikieendesha mashauri nane (8) kwa njia ya hiyo  ikiwa ni mwendelezo.

Mtuhumiwa huyo namba tatu ambaye anakabiliwa na tuhuma ya rushwa na  uhujumu uchumi katika shauri namba 43 la mwaka 2017 la jinai, akiwa na wenzake watano dhidi ya Serikali.

Shauri hilo liletwa mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa,  awali  Mwendesha Mashtaka Wakili wa Serikali, Bi. Ester Martin  alidai kuwa shauri hilo halijakamilika kwa sababu  upelelezi wake haujakamilika na linasubiri kibali kutoka  Ofisi ya  Mkurugenzi wa Mashtaka  nchini (DPP).

Akisoma masharti ya dhamana mahabusu huyo, Hakimu Mkazi Mwandamizi Mhe. Augustina Mmbando alieleza dhamana ya mshitakiwa ipo wazi kwa kuwa na wadhamini wawili watakao weka ahadi ya shilingi milioni Sitini (ml. 60) na mmoja kati yao lazima awe mtumishi wa Umma na kwa pamoja wawasilishe mahakamani hati zao za kusafiria.

Akiahirisha shauri hilo, Mhe. Mmbando alisema litatajwa tena Januari 2, mwaka huu saa tatu   (3; 00) kamili asubuhi.

Mashauri mengine saba  ya jinai yaliyosikilizwa   kwa njia hiyo, ambayo   yako katika hatua ya awali ya kutajwa yote yalihusu Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, kama inavyoelekeza  Sheria Namba Tatu ya mwaka 2016 iliyofanya mabadiliko ya  Sheria ya Uhujumu Uchumi Sura namba 200, ambayo upelelezi wake haujakamilika na mengine yakisubiri kibali kutoka kwa DPP.

Ambapo  shauri la kwanza lilikuwa linamhusu mtuhumiwa  Eke Bidi dhidi ya Serikali, watuhumiwa wengine ni Wolfgang Sylivester, Xiao Shaudan, Hariri Hariri na wenzake, Mohamed Ismail Sued na wenzake, Ally Anguzuu Sharifu na wenzake, Maarifa Abbas Nassor na wenzake na Mohamed Mohamed, wakiwemo wenzake watano wote dhidi ya serikali.

Mashauri hayo yote yatatajwa tena Januari  27, mwaka huu.

Mmoja  wa  wananchi waliofika mahakamani hapo kusikiliza shauri la ndugu yake, Bw. Rajabu Bakari mkazi wa Kongowe alisema  teknolojia ya Mahakama Mtandao ni nzuri ila angependa kumwona ndugu yake uso kwa uso.

Mashauri hayo yenye mahabusu 24 yameendendeshwa mahakamani hapo kupitia gereza hilo kufikia 10, ambapo mawili yaliendeshwa wiki iliyopita Januari 10, mwaka huu.

Uendeshaji  wa mashauri kwa njia hiyo ni mojawapo ya malengo ya Mahakama ya Tanzania ya kuweza kusikiliza mashauri kwa wakati na kupunguza gharama za uendeshaji wa mashauri  hayo mfano  kuwalipa  mashahidi, kuwasafirisha mahabusu, usalama wa mahabusu , zikiwemo nyingine.