Home Mchanganyiko KWANDIKWA: MAKANDARASI ZINGATIENI MAHITAJI YA WATU MAALUM

KWANDIKWA: MAKANDARASI ZINGATIENI MAHITAJI YA WATU MAALUM

0

Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias kwandikwa, akizungumza jambo wakati akikagua jengo la Shoppers jijni Dodoma, ili kukagua ujenzi wake kama umekidhi mahitaji ya watu maalum. Aliyekaa ni Naibu Waziri, Ofisi ya
Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Stella Ikupa, akiwa amaeambatana na Naibu Waziri huyo.

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas Katambi, akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa (aliyevaa kofia) wakati Naibu Waziri huyo alipofika katika jengo la Shoppers jijini Dodoma ili kukagua
kama ujenzi wake umekidhi mahitaji ya watu maalum.

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Stella Ikupa, akizungumza kwa simu na mkandarasi anayejenga jengo la Shoppers jijini Dodoma wakati alipofanya ziara katika jengo hilo ili kukagua jengo hilo kama limekidhi
mahitaji ya watu maalum.

Meneja wa Duka la Shoppers jijini Dodoma, Ashley Fernandes, akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, wakati alipofika katika jengo hilo, ili kukagua kama ujenzi wake umekidhi mahitaji ya watu wenye mahitaji maalum.

******************************

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Elias Kwandikwa ametoa wito kwa makandarasi wanaojenga majengo mbalimbali nchini yanayotoa huduma kwa umma, kuweka miundombinu itakayowezesha watu wenye mahitaji maalum kuingia na kupata huduma hizo katika majengo hayo kwa urahisi.

 

Kwandika ameyasema hayo baada ya kufanya ukaguzi katika duka la Shoppers Plaza lililopo jijini Dodoma na kubaini kasoro ya ujenzi wa kimiundombinu ambayo haikuzingatia mahitaji ya watu maalum katika
jengo hilo.

 

“Kama mnavyoona jengo hili halina eneo la kupita wenzetu wenye mahitaji maalum, pia miundombinu ya vyoo nayo haikidhi mahitaji ya watu hawa, hivyo inakuwa vigumu kwa watu hawa kupata huduma bora hapa”, amesema Naibu Waziri Kwandikwa.

 

Aidha, Naibu Waziri Kwandikwa amewaagiza Bodi ya Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi nchini (AQRB) na Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), kuhakikisha katika michoro yao wanaweka mahitaji ya watu maalum na pia kuongeza wigo wa ukaguzi wa majengo
yanayojengwa ili kubaini mapema na kutatua changamoto za kimiundombinu kabla ujenzi haujaisha.

 

Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kufanya ukaguzi wa majengo nchi nzima lengo ni kuangalia majengo hayo kama yameweka mahitaji kwa watu maalum ikiwemo miundombinu ya njia na vyoo.

 

Kwa upande wake, Naibu Waziri,Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi ,Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Stella Ikupa, amesema kuwa lengo la kufanya ziara zake katika majengo mbalimbali nchini ni kubaini kama majengo hayo yanazingatia mahitaji ya watu maalum.

 

Ameongeza kuwa majengo mengi nchini yamekuwa yakijengwa na kusahau mahitaji ya kundi hilo na hivyo kusababisha kundi hilo na hatimaye kukosa huduma katika maeneo mbalimbali.

 

 

Ameyataja mahitaji hayo kuwa ni miundombinu ya vyoo, njia maalum kwa ajili ya watu wenye ulemavu na eneo maalumu la maegesho ya magari.

 

“Hatupaswi kuendelea kutozingatia mahitaji ya watu hawa, ndio maana mimi mwenyewe naendelea kufanya ziara ya kukagua majengo kama haya ili kuendelea kukumbushia mahitaji yetu, mimi mwenyewe ni
mhanga katika hili kwani wakati mwingine nahitaji kutembea ili kufanya mahitaji yangu”, amesema Naibu Waziri Ikupa.

 

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas Katambi, amesema kuwa kuanzia sasa majengo yote yanayojengwa jijini Dodoma lazima yapate kibali kutoka katika Ofisi zinazohusika na yazingatie kanuni za ujenzi.

 

Amefafanua kuwa wataendelea kukagua na kusimamia kanuni zote za ujenzi ili kuhakikisha majengo yote yaliyopo jijini hapo yanakidhi masharti ya ujenzi.