***********************************
Na Jozaka Bukuku
DESEMBA 12, mwaka jana katika ukumbi wa ofisi za Mkoa wa Pwani Kibaha,Taasisi ya TGT (Tanzania Growth Trust) iliendesha semina ya ujasiriamali kwa wanawake wasiopungua 300 waliopo kwenye makundi ya uzalishaji mali.
Semina hiyo ilifanyika baada ya siku chache kupita tangu taasisi hiyo ichukue tuzo ya umahiri wa kuendeleza watu ambayo ilitolewa na Foundation For Civil Society (FCS) katika kilele cha wiki ya Asasi za kiraia iliyofanyika kuanzia tarehe 3 Novemba 2019 hadi Novemba 8 2019 mjini Dodoma.
Mwaka 2019, ulikuwa na mwanga wa mafanikio kwani mbali na tuzo hiyo iliyopatikana kutokana na mchango wa TGT katika kuboresha maisha ya watu lakini pia walifanikiwa kupanua huduma zao kwa
kusajili Taasisi ndogo ya kifedha ya TGT Microfinance.
TGT inafanya kazi kwa karibu zaidi na makundi ya wazalishajimali ambapo imekuwa ikitoa elimu ya ujasiriamali kwa njia ya vitendo na nadharia,huduma za kifedha na ushauri wa kitalaamu katika njanja
zote za kiuchumi.
Akizungumza kuhusiana na mikakati ya mwaka huu, Afisa Mtendaji Mkuu wa TGT, Bi Anna Dominick amesema kwamba wamefanikiwa kufungua taasisi ndogo ya kifedha ‘’Microfinance’’ ambayo itatanua.
wigo wa huduma za kifedha na kufikia namba kubwa ya wahitaji katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani.
Bi Anna amesema kwamba kuna uhitaji mkubwa wa huduma za kifedha kwa wajasiriamali na wengi wao wanakosa sifa za kukopesheka pindi wanapozisogelea taasisi za kifedha ikiwemo Mabenki hivyo uwepo wa TGT Microfinance utasaidia kupunguza
changamoto hiyo.
Afisa Mtendaji huyo aliongeza kuwa TGT imekuwa na jicho maalumu kwa wanawake na hata programu zake nyingi zimelenga katika kutoa mafunzo, kulea na kuinua miradi ya uzalishaji mali ambayo inatekelezwa na wanawake.
“Wanawake wamekuwa wazalishaji mali wakubwa kwenye jamii zetu hivi sasa na hata ukitazama VICOBA na SACCOSS nyingi zimejaza wanawake ndio maana huduma za kifedha kutoka kwenye taasisi binafsi na Serikali zimekuwa zikiwafikia kwa urahisi’’alisema Bi Anna
Dominick.
Bi Anna anaeleza kuwa Taasisi yake imekuwa ikitoa mwanya wa kupanua masoko ya bidhaa zinazozalishwa na wanawake kwa kuandaa maonesho mbalimbali ya biadhara ili kuwasaidia kuongeza kipato na kutengeneza mitandao ya kibiashara.
“Mbali na mafunzo au huduma za kifedha tunazotoa kwa wanawake lakini pia tumeona twende hatua moja zaidi kwa kuwapa fursa ya kunadi bidhaa na huduma zao kwenye maonesho mbalimbali ikiwemo Saba saba”alimaliza Bi Dominick.
Akizungumzia kuhusu mikakati ya kupanua masoko ya wajasiriamali mwaka huu Bi Dominick amesema kwamba wanatarajia kuandaa maonesho makubwa ya wajasiriamali katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam ambayo yatafanyika kuanzia tarehe 24-28
Februali 2020.
‘’Maonesho ya mwaka huu yatakuwa na sura tofauti kwani mbali na wajasiriamali lakini pia tutashirikisha taasisi za umma ambazo zinahusika na masuala ya urasimishaji wa biashara kama SIDO,BRELLA, TRA,TBS,TMDA, mabenki na wadau wengine’’alimaliza.