*****************************
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia ameteuliwa kuwa Mjumbe wa Kamati Maalum ya kufanyia marekebisho mfumo wa Vyama vya Mpira wa Miguu vya Kikanda barani Afrika (AZA).
Kamati hiyo imeundwa baada ya kikao kati ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) na AZA kilichofanyika hivi karibuni jijini Zurich, Uswisi na kuongozwa na Rais wa FIFA Infantino
Wajumbe wengine wa Kamati hiyo itakayoongozwa na Rais wa CAF, Ahmad Ahmad ni Katibu Mkuu wa CAF, Mouad Hajji, Mario Gallavotti kutoka FIFA, na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu la Niger (NFA), Hamidou Djibrilla.
Mbali ya mfumo, Kamati hiyo itaangalia maeneo mbalimbali kama utawala, waamuzi, makocha, mashindano, ushirikiano na ofisi za kanda za FIFA katika kuendeleza mpira wa miguu hasa katika ngazi ya shule, kuanzisha vyombo vya kinidhamu ambavyo ni muhimu katika mashindano, na misaada ya kiufundi na utawala kutoka FIFA.
Idara ya Wanachama ya FIFA ndiyo itakayoratibu vikao vya Kamati hiyo Maalum ambayo muda wake utakoma baada ya kukamilisha kazi hiyo.
AZA katika kikao hicho iliwakilishwa na viongozi wake kutoka kanda zote sita za mpira wa miguu Afrika. Kanda hizo ni Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Kusini mwa Afrika (COSAFA), Afrika Magharibi (WAFU-A na B), Afrika Kaskazini (UNAF) na Afrika ya Kati (UNIFFAC).
Katika kikao hicho, CAF iliwakilishwa na Rais Ahmad, Katibu Mkuu wake Hajji na Genan Korra, FIFA iliwakilishwa na Rais wa FIFA Gianni Infantino , Veron Mosengo-Omba ambaye ni Mkuu wa Idara ya Wanachama ya FIFA na Solomon Mudege.