******************************
10/01/2020 ZANZIBAR
Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Simon Sirro amewahakikishia hali ya usalama wakazi na wananchi wa Visiwa vya Zanzibar wakati wa sherehe za
miaka 56 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar zitakazofanyika Januari 12 mwaka huu na kwamba yeyote atakayejihusisha na vitendo vya uvunjifu wa
amani atachukuliwa hatua kali za kisheria.
IGP Sirro amesema hayo wakati alipofanya ziara ya ukaguzi wa mradi wa nyumba za makazi ya askari katika mkoa wa Mjini Magharibi na mkoa wa Kusini Unguja pamoja na kufanya ukaguzi katika eneo la uwanja wa mbinu za medani lililopo Kiashanga, Kaskazini Unguja.
Aidha, IGP Sirro ameendelea kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuliwezesha Jeshi hilo kuimarisha miundombinu yake mbalimbali ikiwemo mradi wa ujenzi wa nyumba 400 za makazi ya askari zilizojengwa nchi nzima ambao ujenzi wake tayari umekamilika na askari wameanza kutumia nyumba hizo.