Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akizungumza na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama katika kikao kazi, kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri hiyo leo. Kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Mhe. Emmanuel Luhahula na Katibu Tawala wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, Bi. Elizabeth Rwegasira (kushoto).
Baadhi ya watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) katika kikao kazi kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri hiyo leo
Mbunge wa Jimbo la Mkalama, Mhe. Allan Kiula akiwasilisha hoja za watumishi wa jimbo lake wakati wa kikao kazi kati ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama kilichofanyika leo katika ukumbu wa halmashauri hiyo.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Tatazi iliyo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, Bw.John Cassiano akiwasilisha hoja kuhusu walimu wanaojiendeleza kielimu kutopandishwa vyeo, wakati wa kikao kazi kati ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri hiyo leo.
………………
Na Happiness Shayo, Mkalama-Singida
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) amemuagiza Mkuu wa TAKUKURU
Wilaya ya Mkalama kuchunguza utendaji wa Kitengo cha Manunuzi cha
Wilaya hiyo kutokana na utekelezaji mbovu wa miradi ya maendeleo.
Agizo hilo amelitoa leo wakati wa kikao kazi na watumishi wa Halmashauri
ya Wilaya ya Mkalama kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri hiyo.
“Nataka TAKUKURU mkichunguze Kitengo cha Manunuzi cha Wilaya ya
Mkalama kwa sababu nimebaini kuna mwenendo mbaya katika utekelezaji
wa miradi hapa wilayani” Dkt. Mwanjelwa amesema.
Amefafanua kuwa Kitengo hicho kimekuwa kikitoa tenda za miradi
mbalimbali bila kufuata utaratibu ikijumuisha pia upotevu wa vifaa vya
ujenzi katika mazingira ya kutatanisha.
Dkt. Mwanjelwa ameweka bayana kuwa Serikali ya Awamu ya Tano
imekuwa ikijitahidi kuhakikisha inafikisha huduma karibu na wananchi
akitolea mfano ujenzi wa hospitali, upanuzi wa vituo vya afya na ujenzi wa
masoko, lakini wako baadhi ya watumishi wanaofanya ubadhirifu.
“Natoa onyo kwa watumishi ambao bado wanafikiria kujipatia fedha kupitia
miradi hii na ninawapa pole kwa sababu Serikali ya Awamu ya Tano
inayoongozwa na Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli haitaki mzaha katika
utendaji kazi ”Dkt. Mwanjelwa ameongeza.
Amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inataka watumishi walio safi
kiutendaji, wanaowajibika ipasavyo na wanaofanya kazi kwa kufuata
kanuni na taratibu za kiutumishi.
Katika hatua nyingine, Dkt. Mwanjelwa amemuelekeza Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama kutekeleza agizo la serikali la
kuwaondoa kazini watumishi wenye vyeti vya kughushi.
Maelekezo hayo ameyatoa baada ya kupokea malalamiko ya Mwalimu
Mkuu wa Shule ya Msingi Malela, Bw. Alfred Panda aliyetaka kujua hatima
ya mmoja wa walimu wake aliyebainika kuwa na cheti cha kughushi wakati
wa zoezi la kusafisha taarifa za watumishi, lakini amekuwa akiendelea na
kazi na amefuatilia barua yake ya kusimamishwa kazi bila mafanikio.
Dkt. Mwanjelwa amemtaka Mkurugenzi wa Halmashuri ya Wilaya ya
Mkalama kulifanyia kazi suala la mtumishi huyo haraka iwezekanavyo.
“Mkurugenzi hakikisha hatua kali za kisheria zinachukuliwa haraka kwa
mtumishi huyu ambaye ana vyeti feki na unipe mrejesho” Dkt. Mwanjelwa
amesisitiza.
Mhe.Dkt. Mwanjelwa yupo Mkoani Singida katika ziara ya kikazi yenye
lengo la kukagua utekelezaji wa shughuli za TASAF pamoja na kukutana na Watumishi, kusikiliza maoni kero zao na kuzitatua.