NA MWAMVUA MWINYI, BAGAMOYO
WAKAZI wa Vijiji vinavyounda Kata ya Zinga, Bagamoyo ,Mkoani Pwani, ambao hawajalipwa fidia katika mradi wa EPZ wamemfikishia kero yao mke wa Rais Mstaafu wa Serikali ya awamu ya nne Mama Salma Kikwete, wakidai wapewe maeneo yao ili kujiendeleza kimaendeleo.
Wamemueleza kuwa, mara kadhaa wamekuwa wakiomba suala hilo na kudai kwamba ni kitendo ambacho ni kama ni kupuuzwa agizo la Rais John Magufuli, la kuwataka wananchi hao wapewe maeneo yao.
Kilio hicho kimetolewa na Mwenyekiti wa Jumuia ya Wazazi katika kata hiyo , Mukhisin Mintanga, wakati Mama Salma Kikwete, akiwa katika ziara ya kuimarisha Jumuiya ya Wanawake (UWT) wilayani humo.
Mintanga alisema, pamoja na kauli ya Rais Magufuli , lakini hakuna utekelezaji wake.
“Rais Magufuli alipokuja alitoa agizo kwamba, wananchi ambao hawajalipwa fidia kupisha mradi wa EPZ waruhusiwe kuendeleza maeneo yao, lakini wanapokwenda halmashaauri au ofisi za EPZ wanambiwa maeneo yamewekewa GN, mpaka itenguliwe na Waziri mwenye dhamana,” alisema Mintanga.
Nae mbunge wa Jimbo la Bagamoyo Dkt. Shukuru Kawambwa alimwambia Mama Salma kwamba, suala hilo alishaanza kulifanyikazi, lakini kwa bahati mbaya Waziri aliyekuwepo amebadilishwa Wizara, hivyo amewasiliana na Waziri Biteko aliyeshika nafasi hiyo, kuhusiana na suala hilo.
“Mheshimiwa Mama Salma suala hili awali lilinichanganya, nikahoji hivi ni nani aliye juu ya Rais, sababu Rais Magufuli ameshaagiza kuwa waliokosa fidia wapewe maeneo yao lakini hakuna utekelezaji, ndipo nikaelezwa kuwa kuna hatua za kufuatiliwa wizarani kuhusiana na GN,” alisema Dkt. Kawambwa.
Kwa upande wake ,mama Salma alibainisha ameichukua kero hiyo, na kuwa ataungana na Mbunge Kawambwa katika kulifanyiakazi, ili agizo lililotolewa na Rais liweze kutekelezwa mapema iwezekanavyo.
Wakati huo huo,Mama Salma aliwataka wakazi wilayani hapa kushiriki zoezi la uboreshwaji wa daftari la makazi, linalotaraji kuanza tarehe moja mwezi wa pili, litalodumu kwa siku saba .
Ziara ya Mama Salma iliyoanzia Jimbo la Chalinze na kumalizia Bagamoyo, akiwa Zinga amepokea changamoto kadhaa ikiwemo ya fidia.